John Magufuli Alazwa, Abbasi Mtemvu Apata Ajali
Na Mwandishi Wetu Dodoma
WAZIRI wa Ujenzi, Dk. John Magufuli(pichani juu kulia), amelazwa
katika hospitali ya Mkoa wa Dodoma baada ya kufikishwa akisumbuliwa na ugonjwa
wa shinikizo la damu
Naibu Spika wa Bunge, Bw Job Ndugai, alitoa
taarifa hiyo muda mfupi kabla ya kuahirisha Bunge jana mchana ambapo wabunge
walishikwa na taharuki baada ya kusikia taarifa hiyo.
Alisema hadi jana afya ya Waziri Magufuli ilikuwa
inaendelea vizuri kutokana na matibabu aliyopewa na kuwaomba watanzania
waendelee kumuombea ili apone haraka. “
asubuhi zililetwa taarifa hapa, kwamba mwenzetu Dk. Magufuli anaumwa na
amekimbizwa katika Hospitali ya Mkoa Dodoma kwa matibabu”alisema Bw Ndugai.
“Taarifa nilizonazo ni kwamba, alipofikishwa
hospitalini na kupimwa, ilionekana ‘preasure’ (shinikizo la damu) lilikuwa
juu. Alisema kuwa tayari Waziri
Mkuu,Mizengo Pinda alikwenda kumjulia hali hospitalini na kueleza kuwa hali
yake inaendelea vizuri, preasure imeshuka ila bado anaendelea kusumbuliwa na
vichomi.
Aidha Naibu Spika pia aliliambia Bunge, kuwa
Mbunge wa Temeke, Abas Mtemvu (CCM)(pichani chini kulia), amepata ajali ya barabarani mkoani
Morogoro. Alisema ajali hiyo ilitokea
jana saa 12.15 asubuhi baada ya gari la mbunge huyo kugongwa na roli alipokuwa
akitoka Mjini Dodoma kuelekea jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Naibu Spika, Mtemvu na dereva wake
walipata majeraha na kutibiwa mkoani humo kabla ya kuendelea na safari kuelekea
Jijini Dar es Salaam kwa matibabu zaidi. Katika ajali hiyo, alisema gari la
Mtemvu liliharibiwa vibaya.
No comments:
Post a Comment