Sunday, April 01, 2018

MHAGAMA: MIRADI YA MWENGE WA UHURU KUKAGULIWA KISAYANSI...OLE WAO MA-DED

PICHANI: Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu- Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Jenista Mhagama (wa tatu kushoto), akizungumza na kamati mbalimbali za maandalizi ya Mwenge wa Uhuru kitaifa. Kikao hicho kilichofanyika Machi 31, 2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, pia kilishirikisha waandishi wa habari. Mwenge wa Uhuru unaanza mbio zake kesho Aprili 2, 2018 mkoani Geita. Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel (wa pili kushoto) na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Alhaj Said Kalidushi. (Picha na Yusuph Mussa)

Na Yusuph Mussa, Geita
Immamatukio Blog

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu- Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama, amezionya halmashauri zote nchini zikae mguu sawa, kwani vijana watakaokimbiza Mwenge wa Uhuru kitaifa, mwaka huu, wamepewa mafunzo ya kubaini thamani ya miradi na ulinganifu wa fedha zilizotumika.

Hivyo halmashauri zisije 'zikachakachua' miradi hiyo kwa kutaja viwango vikubwa vya fedha zilizotumika ama kuwa chini ya kiwango, wakurugenzi wake na wahusika wote hawatabaki salama. Kwani nia ya Serikali na falsafa ya Mwenge wa Uhuru, mojawapo ni kuangalia miradi, lakini na uzalendo mbele katika kujenga miradi hiyo.

Aliyasema hayo jana Machi 31, 2018 kwenye kikao cha wadau kwa ajili ya maandalizi ya Mbio za Mwenge wa Uhuru zinazoanza kesho Aprili 2, 2018 mkoani Geita. Kikao hicho ambacho kimewashirikisha viongozi wa kamati mbalimbali za maandalizi hayo pamoja na waandishi wa habari, kilifanyika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.
"Safari hii miradi ya Mwenge wa Uhuru itakaguliwa kisayansi. Na hapo kwenye miradi ndipo kwenye ukaguzi kweli kweli. Tutaangalia kila senti iliyokusanywa kwa miradi inayoiingizia fedha halmashauri au fedha iliyotumika kwa miradi ya maendeleo inayotekelezwa, na kuona thamani ya miradi kama inaendana na matumizi ya fedha.

"Tuna kikosi kizuri sana (wakimbiza Mwenge wa Uhuru kitaifa) ambacho kimeiva kwa kazi zote ikiwemo kukagua miradi, kutangaza ujumbe wa Mwenge wa Uhuru na kuelezea falsafa ya Mwenge wa Uhuru" alisema Mhagama.

Mhagama alisema bado nchi yetu inauhitaji Mwenge wa Uhuru, kwani mawazo ya Mwalimu Julius Nyerere ya kuutaka Mwenge wa Uhuru kuwa sehemu ya kuleta matumaini na kuondoa chuki, kujenga umoja, mshikamano na kuwa na amani ya kudumu, kwa sasa ni muhimu zaidi.

"Falsafa ya Baba Taifa Mwalimu Nyerere, ya kuwasha Mwenge wa Uhuru na kuuweka kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro, bado ipo. Bado tunahitaji umoja, mshikamano, kulinda amani na kuwa wazalendo. Hivyo lazima tuendelee kuenzi falsafa ya Mwalimu Nyerere kwa kuendelea kukimbiza Mwenge wa Uhuru" alisema Mhagama.

Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel alisema ni dhamana kubwa wamepewa na Serikali kuwa wenyeji wa Mwenge wa Uhuru kitaifa, hivyo nia na dhamira yao ni kuona wanafanikisha maandalizi ya Mwenge wa Uhuru na kuweza kukimbizwa nchini kote.

"Tumejipanga kila kamati husika, kila idara husika na mtu mmoja mmoja. Nia yetu ni kuona tunafanikisha jambo hili zito tulilokabidhiwa na Taifa kulitenda. Nawaomba wahusika, nisije nikampigia simu mtu akasema nilikuwa nasali ama simu haina chaji. Wala kusema Mkuu wa Mkoa nilikupigia, lakini ulikuwa hupatikani. Kuanzia leo simu zangu zote zitakuwa full charge na wewe iwe vivyo hivyo" alisema Mhandisi Gabriel.

Katika mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2017, miradi 21 katika halmashauri 19 nchini, ilikataliwa.

Baadhi ya wadau wa Mwenge wa Uhuru Geita (Kamati za maandalizi na waandishi wa habari) wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu- Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Jenista Mhagama (hayupo pichani) kwenye kikao kilichofanyika Machi 31, 2018 kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita. Mwenge wa Uhuru unaanza mbio zake kesho Aprili 2, 2018 mkoani Geita. (Picha na Yusuph Mussa).Baadhi ya wadau wa Mwenge wa Uhuru Geita (Kamati za maandalizi na waandishi wa habari) wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu- Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Jenista Mhagama (hayupo pichani) kwenye kikao kilichofanyika Machi 31, 2018 kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita. Mwenge wa Uhuru unaanza mbio zake kesho Aprili 2, 2018 mkoani Geita. (Picha na Yusuph Mussa).

No comments:

Post a Comment