Wilaya wanapoishi watoto zina mchango mkubwa katika kujifunza: tofauti ya ufaulu kati ya wilaya bora na zile za mwisho ni asilimia 60
Wilaya zinatofautiana sana katika upatikanaji wa vifaa na huduma shuleni
27 Februari 2018, Dar es Salaam: Miongoni mwa watoto wenye umri wa miaka 9 hadi 13, asilimia 38 hawawezi kufanya majaribio ya darasa la 2 huku tofauti kubwa ikionekana kwenye wilaya. Wilaya ya Iringa Mjini, inayoongoza kwa ufaulu, asilimia 75 ya watoto wenye umri wa miaka 9 hadi 13 wana uwezo wa kufaulu majaribio ya kusoma Kiingereza na Kiswahili na kufanya hesabu za darasa la pili. Lakini wilayani Sikonge ni asilimia 17 tu ya watoto walioweza kufaulu majaribio hayo.
Asilimia 64 ya watoto mkoani Dar es Salaam wenye miaka 9 hadi 13 wana uwezo wa kufaulu majaribio yote matatu, lakini mkoani Katavi, ni asilimia 23 tu ya watoto wanaoweza kufaulu majaribio hayo. Aidha, watoto wawili kati ya kumi (asilimia 16) wenye umri wa miaka 11 wako nyuma kimasomo mkoani Dar es Salaam. Mkoani Katavi, idadi hiyo ni watoto saba kati ya kumi.
Tofauti kubwa zinabainika pia katika vifaa, rasilimali na huduma zipatikanazo shuleni.
· Mkoani Dar es Salaam, nusu ya shule (asilimia 51) zina huduma ya umeme, lakini mkoani Geita, ni shule 2 tu (asilima 4 tu) kati ya 50 zinazopata huduma hiyo.
· Mkoani Geita, shule moja tu kati ya kumi (asilimia 12) ina huduma ya maji safi na salama, lakini mkoani Kilimanjaro, karibu shule 8 kati ya 10 (asilimia 78) zina huduma hiyo.
· Mkoani Kilimanjaro, wanafunzi 26 wanatumia choo kimoja, ukilinganisha na mkoani Geita ambapo wanafunzi 74 wanatumia choo kimoja.
· Vile vile, asilimia 5 ya shule mkoani Geita zinatoa huduma ya chakula cha mchana wakati mkoani Kilimanjaro ni asilimia 79.
· Mkoa wa Dar es Salaam, wanafunzi sita wanatumia kitabu kimoja wakati mkoani Kilimanjaro, wanafunzi wawili tu wanatumia kitabu kimoja.
· Mkoani Kilimanjaro mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi 36, lakini Katavi, mwalimu huyo mmoja anafundisha wanafunzi 52.
Meneja wa Uwezo (Tanzania) iliyoko Twaweza, Zaida Mgalla, anasema “Takwimu za Uwezo zinaonesha wazi kuwa, kukosekana kwa usawa kwenye mfumo wa elimu, kunajidhihirisha katika matokeo ya kujifunza, rasilimali na huduma zinazopatikana shuleni. Habari njema ni kwamba sasa tuna mifano hai ya nini kinachopaswa kufanyika ili kurekebisha hali hii hapa nchini. Serikali inapaswa kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha kuwa watoto na wilaya za mwisho haziachwi nyuma.”

No comments:
Post a Comment