Monday, February 26, 2018

ASKARI MAGEREZA 11 WASOMEWA MASHTAKA YA MAUAJI KOROGWE

ASKARI magereza 11 waliopo Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga wamefikishwa Mahakama ya Wilaya ya Korogwe na kusomewa mashitaka wakituhumiwa kumuua mwananchi wa Kijiji cha Kerenge, Kata ya Kerenge wilayani Korogwe.

Akisoma shitaka hilo leo (Feb. 26) Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Manundu, Albert Nyang'ali, ambaye alisoma shitaka hilo la mauaji kama Mlinzi wa Amani kwenye Mahakama ya Wilaya ya Korogwe, alisema watuhumiwa hao wanadaiwa kumuua Aloyce Makala wa kijiji cha Kerenge.

Nyang'ali aliwataja askari hao kuwa ni P. 5377 Inspekta Makere, A. 4921 RSM (Mkuu wa Nidhamu Mokiwa Shadrack Lugendo, A. 7367 Sajenti Mussa Mdoe Seif, B. 5919 Koplo Lazaro Stephen Nyato, B. 5486 Koplo Ramadhan Yusuph, B. 7087 WDR Robert Alfred, B. 7980 Fidirishi Cosmas Joseph, B. 7248 WDR Alphonce Revocatus, B. 8911 WDR Mbesha Naftari, B. 9747 WDR Michael Elias Michael na B. 8533 WDR Hamis Halfa Msola.


Nyang'ali alisema watuhumiwa wote kwa pamoja wamedaiwa, mnamo Januari 22, 2018 katika kijiji cha Kerenge wilayani Korogwe walimuua Aloyce Makala maarufu kama Mapi. Katika kesi hiyo namba 2 P I ya mwaka 2018, watuhumiwa wote wamekana shitaka, lakini hawakutakiwa kujibu chochote kwa vile Mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi ya mauaji.

Shauri hilo limepangwa kutajwa tena Machi 12, mwaka huu. Na hii ni mara ya tatu kesi hiyo inatajwa bila kusikilizwa kwa vile jalada la kesi hiyo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kwa hatua muhimu za kiuchunguzi, na watuhumiwa wote wamerudishwa rumande.

No comments:

Post a Comment