Wednesday, December 20, 2017

TANESCO YALIA NA WAHARIBIFU WA MAZINGIRA KATIKA VYANZO

Na Mwandishi Wetu, Mtera

MABADILIKO ya tabia nchi, uharibifu mkubwa wa mazingira utokanao na shughuli za kibidanamu pembezoni mwa mito inayoingiza maji katika Bwawa la Mtera, unachangia kupunguza ufuaji umeme katika bwawa hilo.

Bwawa hilo lipo mpakani mwa Mkoa wa Iringa na Dodoma, lilianzishwa mwaka 1888 kwa lengo la kuhifadhi maji ya ufuaji umeme katika Kituo cha Kidatu, mkoani Morogoro. Kaimu Meneja wa Kituo hicho, kutoka Shirika la Umeme nchini (TANESCO), Mhandisi David Myumbilwa, aliyasema hayo juzi alipozungumza na Wahariri wa vyombo vya habari.

Wahariri hao wapo katika ziara ya kutembelea vituo vyote vinavyozalisha umeme kwa njia ya maji ambao ni rahisi na kujionea changamoto. Alisema pamoja na uhaba wa maji uliopo katika bwawa kutokana na sababu hizo, kituo hicho kimeendelea kufua megawati 80 za umeme wanazopawa kuzalisha.

Aliongeza kuwa, bwawa hilo linapokea maji kutoka Mto Ruaha Mkubwa na Mdogo pamoja na Mto Kizigo uliopo mkoani Singida. "Uzalishaji umeme wa kutosha unahitaji wingi wa maji ambayo kiwango cha juu ili mitambo iweze kuzunguka vizuri ni ujazo wa 698.5, chini ya hapo ikifika 690 tunazima mitambo kwa sababu ya usalama wa mashine," alisema.

Kwa upande wake, Mtaalamu wa Mazingira kutoka TANESCO, Yusuf Kamote, alisema athari nyingi za kimazingira zinazofanywa na binadamu, shughuli za kilimo pembezoni mwa mito muhimu pamoja na ufugaji, zinachangia kupunguza ufuaji umeme unaofanywa na TANESCO.

"Shirika limekuwa likifanya kazi kubwa ya kutoa elimu kwa wakulima na wafugaji ili wasiendelee kuharibu vyanzo vya maji, kuliwezesaha shirika liweze kuzalisha umeme wa uhakika," alisema.

Alisema uharibifu wa mazingira unaofanyika katika mito ambayo ni vyanzo muhimu vya ufuaji umeme una athari kubwa kwa TANESCO ambayo italazimika kusitisha ufuaji umeme.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja Uhusiano wa TANESCO, Leila Muhaji, alisema lengo la ziara ni kuwapa uelewa Wahariri kuhusu uwekezaji uliofanywa na Serikali katika sekta hiyo. Alitoa wito kwa wananchi waishio pembezoni mwa vyanzo vya maji kuona umuhimu wa kuvitunza ili viendelee kuleta manufaa kwa jamii na Taifa hasa katika uzalishaji wa nishati ya umeme.


No comments:

Post a Comment