Thursday, November 23, 2017

WAZIRI WA MAJI ATOA AGIZO ZITO

PICHANI: Waziri wa Maji Mhandisi Issack Kamwelwe akifungua Kongamano la tano la Wadau wa Maji nchini linalofanyika kwa siku mbili Novemba 23 na 24, 2017 jijini Tanga. (Picha na Yusuph Mussa).


Na Yusuph Mussa, Tanga

WAZIRI wa Maji Mhandisi Issack Kamwelwe ameziagiza halmashauri zote nchini, hadi Juni 30, 2018 ziwe zimevuka asilimia 75 ya upatikanaji wa maji mijini na vijijini.

Alisema Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inajieleza wazi kuwa maji yatapatikana umbali usiozidi mita 400, hivyo tunapozungumzia nchi ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo 2025, lazima maji yapatikane.

Aliyasema hayo leo (Nov. 23) wakati anafungua Kongamano la tano la Wadau wa Maji ambalo linawahusisha wadau mbalimbali ikiwemo wataalamu na viongozi kwenye halmashauri zote nchini na kufanyika Jiji la Tanga kwa siku mbili Novemba 23 na 24, 2017.

PICHANI KUSHOTO: Wadau wakifuatilia Kongamano la Tano la Wadau wa Maji nchini linalofanyika jijini Tanga. (Picha na Yusuph Mussa).

"Ilani ya CCM inaagiza maji yapatikane umbali usiozidi mita 400. Na tunapozungumzia uchumi wa viwanda, basi tumtue ndoo kichwani ili huyu mama afanye kazi nyingine. Na Tanga ambayo ina mikakati ya viwanda na miradi mikubwa (ikiwemo Bomba la Mafuta kutoka Uganda), maji ni muhimu.

" Naagiza hadi Juni 30, 2018 halmashauri zote ziwe zimevuka asilimia 75 ya upatikanaji maji. Kama mtaalamu au kiongozi una mipango na mikakati ya kutuwezesha kupata naji, lete tutaifanyia kazi" alisema Mhandisi Kamwelwe.

Kamwelwe amesema hata wataalamu wa mipango miji, wanatakiwa kubainisha na kuweka miundombinu ya maji kwa ajili ya binadamu, mifugo na maeneo ya viwanda ili kurahisisha ujenzi wa viwanda na kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji.

Kamwelwe amekiri, uharibifu wa vyanzo vya maji pamoja na matumizi mabaya ya maji, kumechangiwa hadi sasa huduma ya maji nchini kupatikana kwa asilimia 55 tu, hivyo mikakati inawekwa kulinda vyanzo vya maji na kuongeza miradi ya maji.

"Mwaka 2006/07 miradi ya maji ilikuwa 1,810, lakini iliyokamilika ni 1,433 na inayotoa maji ni 1,017 sawa na asilimia 65. Na Awamu ya Pili ya ujenzi wa miradi ya maji itakuwa 4,105" alisema Kamwelwe.

No comments:

Post a Comment