Saturday, November 25, 2017

ANNE KILANGO AMPIGIA DEBE MGOMBEA UDIWANI KOROGWE


PICHANI: Mbunge wa kuteuliwa na Rais, Anne Kilango Malecela akimnadi mgombea udiwani kata ya Majengo Halmashauri ya Mji Korogwe mkoani Tanga leo hii Mustapha Shengwatu (Picha na Yusuph Mussa).

 Na Yusuph Mussa, Korogwe

MBUNGE wa kuteuliwa na Rais, Anne Kilango Malecela amewataka wananchi wa kata ya Majengo katika Halmashauri ya Mji Korogwe kumchagua mgombea udiwani kupitia CCM Mustapha Shengwatu, kwani watakuwa wamekamilisha safu ya kuwaletea maendeleo.

Akizungumza kwenye mkutano wa ufungaji wa kampeni leo (Novemba 25) kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Boma, amesema ili kusukuma maendeleo ni lazima viongozi wote kuanzia kata, halmashauri na Taifa kuimba wimbo mmoja, na wasikubali kumchanganyia Mbunge wa Korogwe Mjini Mary Chatanda mtu ambaye sio CCM.

"Wananchi wa Majengo msidanganyike. Kwanza tayari tumepata Rais Dkt. John Magufuli ambaye anawajibika ipasavyo ili kuwaletea wananchi maendeleo. Lakini pia mmepata Mbunge mahiri Mary Chatanda. Hivyo msije mkachanganya diwani kutoka chama kingine, huyo hataweza kwenda na kasi ya viongozi hawa.

" Na ili fedha za miradi ziweze kusimamiwa vizuri ngazi ya kata, uhakika ni kuwa na diwani kutoka chama tawala ili kuweza kusukuma mandeleo ya pamoja na kuondoa msuguano wa mara kwa mara" alisema Kilango.

Chatanda aliwataka wananchi kumchagua Shengwatu kwa vile anatosha na ana kazi zake za kufanya, hivyo hata Serikali ikimkabidhi fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya kata yake zitakuwa salama.

Chatanda alisema wamepiga hatua katika jitihada za kuwaletea wananchi maendeleo, kwani kero kubwa ya maji inakaribia kubaki historia pale mradi wa maji Mtonga utakapokamilika Desemba, mwaka huu sambamba na ule wa Old Korogwe.

Alisema pia wanajenga Kituo cha Afya Majengo cha ghorofa tatu, ambapo Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alipofanya ziara Korogwe, aliahidi kama Serikali kuchangia sh. milioni 300, ni baada ya kuelezwa kituo hicho kinajengwa kwa nguvu za wananchi.

"Kama hautoshi, Rais Dkt. Magufuli alipofanya ziara kwa ajili ya kufungua Stendi Kuu ya Mabasi Korogwe (Agosti 7, 2017), aliongeza sh. milioni 350 ili kuunga mkono jitihada za wananchi kujenga kituo hicho.

" Lakini pia tulipata bahati kwa aliyekuwa Mkuu wetu wa Wilaya Mhandisi Robert Gabriel kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita, hiyo yote ni kutokana na ushirikiano tuliokuwa nao kati ya Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Korogwe Jumanne Shauri na mimi Mbunge" alisema Chatanda.

PICHANI: Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini mkoani Tanga Mary Chatanda akimnadi mgombea udiwani kata ya Majengo Mustapha Shengwatu leo hii kwenye ufungaji wa kampeni katika viwanja vya Shule ya Msingi Boma. (Picha na Yusuph Mussa).
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Tanga na Mkuu wa Mkoa huo Martin Shigela aliwataka wananchi kumchagua Shengwatu ili kuunganisha mnyororo wa uongozi bora, na hiyo ni kutokana na sera nzuri za CCM.

Mchuano mkali kwenye uchaguzi wa kesho unatarajiwa kuwa mkali kati ya Shengwatu wa CCM na Abdallah Maonga wa CHADEMA. Uchaguzi huo mdogo unafanyika baada ya aliyekuwa Diwani wa Kata ya Majengo Idd Mhina wa CCM kupoteza sifa ya kuendelea na nafasi hiyo. Jimbo la Korogwe lina kata 11, ambapo kabla ya uchaguzi huo, zote zilikuwa CCM.




No comments:

Post a Comment