Tuesday, October 03, 2017

WATUMISHI HEWA WAMEDUMAZA HUDUMA ZA JAMII

PICHANI: Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli akifurahia jambo na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Mhe Isaya Mwita baada ya kuzindua mkutano wa 33 wa ALAT katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere Dar es Salaam leo (picha ya mtandao)

Na Yusuph Mussa

Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli amesema watumishi hewa wamechangia kudumaza huduma za kijamii na miradi ya maendeleo kutokana na fedha hizo kulipwa kwa watu ambao hawakustahili.

Amesema watumishi hewa hao hawakuja kwa bahati mbaya, bali kulikuwa kuna wajanja wachache ndani ya mfumo wa Serikali ambao walikuwa wananufaika na hilo.

Aliyasema hayo leo Oktoba 3 wakati anahutubia wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 33 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) unaofanyika kwa siku tano kuanzia Oktoba 2 hadi 5, 2017 kwenye Kituo cha Mikutano cha Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.



PICHANI KULIA: Baadhi ya Wajumbe wa ALAT Taifa walioshiriki mkutano huo.

Rais Dkt.Magufuli alisema pamoja na watumishi hewa pia kulikuwa na wenye vyeti vya kughushi, ambao kwa namna moja ama nyingine, nao walikuwa wanapata mishahara wasiyostahili, lakini pia wamesababisha watu kupuuza kujiendeleza kielimu, kwani walikuwa na uhakika wa kupata pesa.

"Watumishi hewa 20,000 kwa mwezi walikuwa wanalipwa sh. bilioni 19.8, hivyo kwa mwaka walikuwa wanalipwa sh. bilioni 238.1. Hawa watu hawakuwa kwenye vitabu, lakini kila mmoja alikuwa na mtu wake serikalini anamlinda.

"Pesa hizi ni nyingi, na zingeweza kulipa posho madiwani, kujenga vyoo vya wanafunzi wetu, kununua dawa ama kujenga nyumba za walimu. Lakini kuna watu walikuwa wanalipana fedha hizo, kwangu ni kama kuzitupa chooni" alisema Dkt. Magufuli.

Dkt. Magufuli alisema mishahara hewa ilikuwa inaendana na likizo za uzazi hewa, likizo za kawaida hewa na pensheni hewa, hivyo kuagiza fedha za pensheni sh. bilioni 38 zilizolipwa kama pensheni kwa watumishi hewa, zirudishwe serikalini.

Alisema mapambano hayakuwa kwenye watumishi hewa tu, kwani wenye vyeti vya kughushi zaidi ya 12,000 walikuwa wanalipwa sh. bilioni 11.9 kwa mwezi, na kwa mwaka walikuwa wanalipwa sh. bilioni 142.9 kwa mwaka.

"Hivyo wafanyakazi hewa 20,000 na wenye vyeti vya kutengeneza Kariakoo 12,000 wote kwa mwaka walikuwa wanalipwa sh. bilioni 381. Hawa wote walikuwa wanazorotesha ufanisi na kuondoa ari ya kuwajibika. Lakini wenye haki walikuwa hawapati fursa" alisema Dkt. Magufuli.


No comments:

Post a Comment