Friday, October 13, 2017

UHARIBIFU MIUNDOMBINU, TANESCO YAINGIA HASARA YA MAMILIONI

Na Mwandishi Wetu, Songea

UHARIBIFU wa miundombinu ya Shirika la Umeme nchini (TANESCO), unaofanywa na baadhi ya watu mkoani Ruvuma, husababisha shirika hilo kuingia hasara ya mamilioni ya fedha na kukwamisha huduma ya upatikanaji umeme kwa wateja.

Changamoto kubwa inayolikabili shirika hilo ni uchomwaji nguzo zinazopitisha umeme kwenye maeneo ya vijijini na pembezoni mwa barabara ambako kuna miundombinu ya TANESCO. Uharibifu huo hufanywa na baadhi ya wananchi ambao huchoma moto mashamba yao wakati wa kuyaandaa ili kuanza msimu wa kilimo bila kuchukua tahadhari.

Meneja anayesimamia mradi mkubwa wa umeme unaotoka Makambako, mkoani Njombe-Ruvuma, Mhandisi Didas Lyamuya (Pichani, mbembeni ya moja ya nguzo zilizounguzwa na moto), alisema changamoto hiyo ni kikwazo kwa shirika kutoa huduma ya umeme wa uhakika kwa wateja.


Mhandisi Lyamuya aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na Wahariri wa vyombo vya habari walio katika ziara ya kuangalia uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kupitia TANESCO kwenye sekta ya umeme nchini.

Alisema uharibifu huo umefanywa katika nguzo zinazosafirisha umeme kwa kuchomwa moto na nguzo mpya za mradi wa Makambako-Songea ambao unaendelea kutekelezwa.


Aliwaomba viongozi wa Serikali ya vijiji, kutoa elimu kwa wananchi wao ili waone umuhimu wa kuitunza miundombinu hiyo ili kuliepusha shirika na hasara kubwa wanayoipata. "Lengo la TANESCO ni kufikisha huduma ya umeme kwa wananchi, kuharakisha maendeleo yao na kufungua fursa ya ujenzi wa viwanda," alisisitiza Mhandisi Lyamuya.

Kaimu Meneja Uhusiano wa TANESCO, Leila Muhaji, alitoa wito kwa wananchi na viongozi wa vijiji kuilinda miundombinu ya shirika hilo kwani Serikali inatekeleza miradi hiyo kwa faida yao.

No comments:

Post a Comment