Na Mwandishi Wetu, Mtwara
SERIKALI kupitia Shirika la Umeme nchini (TANESCO), iko mbioni kununua jenereta mbili zenye uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati nne (4MW), ili kwenda sambamba na ongezeko la matumizi ya umeme kwa wateja.
Jenereta hizo zitasaidia kuboresha hali ya upatikanaji umeme katika Mkoa huo na Lindi ambao unapokea umeme kutoka Mtwara. Umeme huo unazalishwa kwenye kituo kipya cha kupoozea umeme kilichopo eneo la Mdenga, kikipokea umeme wa 132/33kV kutoka kituo cha ufuaji umeme kwa kutumia gesi asilia cha Mtwara Power Plant.
Kituo hicho cha kupoozea umeme kilizinduliwa na Rais DKt. John Magufuli, Machi 5, mwaka huu, kikiwa na transfoma yenye uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 30.
Meneja wa mradi huo, Mhandisi Jafari Msuya, aliyasema hayo mjini Mtwara jana alipozungumza na Wahariri kutoka vyombo mbalimbali waliopo kwenye ziara ya kuangalia uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kupitia TANESCO kwenye sekta ya umeme nchini.
Alisema mahitaji ya umeme unaozalishwa katika kituo hicho kwa Mtwara ni megawati 11 naeLindi megawati tano. Aliongeza kuwa, ujenzi wa kituo hicho ulikwenda sambamba na ujenzi wa njia kuu ya kusafirishia umeme kutoka Mtwara hadi Lindi msongo wa 132 kV na kituo cha kupoozea umeme cha Lindi kinachoitwa Mahumbika.
Maeneo yaliyonufaika na mradi huo ni Manispaa ya Mtwara, Wilaya za Tandahimba, Newala, Masasi pamoja na Nanyumbu. Kwa Manispaa ya Lindi ni Wilaya za Lindi Vijijini, Nachongwea, Ruangwa na baadhi ya vijiji vya Wilaya ya Kilwa, mkoani humo.
"Mradi huu ukijumuisha ujenzi wa vituo vya kupoozea umeme na njia kuu ya kusafirishia umeme umegharimu sh. bilioni 16.
"Fedha hizi zimetolewa na Serikali ya Tanzania, ujenzi wa njia kuu msongo wa 132 kV umefanywa na Kampuni tanzu ya TANESCO iitwayo ETDCO iliyoanzishwa hivi karibuni kwa kushirikisha wataalamu wa shirika," alisema.
Akizungumza faida za mradi, alisema ni pamoja na kuimarisha upatikanaji umeme katika mikoa hiyo ambapo awali, umeme msongo wa 33 kV kutoka Mtwara-Lindi ulisafirishwa umbali wa kilomita 100, baada ya mradi umefupishwa na kuwa kilomita 20.
Umeme uliozalishwa kutoka Mtwara hadi Ruangwa, ulisafirishwa umbali wa kilomita 300, baada ya zimepungua na kuwa kilomita 120. Alitoa wito kwa wakazi wa Mtwara na Lindi ambao mradi huo umepita katika maeneo yao, kutoa ushirikiano kama walivyofanya wakati wa ujenzi kwa kulinda miundombinu ya umeme.
No comments:
Post a Comment