Friday, September 29, 2017

SHIRIKA LA POSTA TANZANIA (TPC) LAKUTANA NA MSAJILI WA HAZINA



Msajili wa Hazina, Dkt. Oswald Mashindano (katikati), akiueleza jambo uongozi wa Shirika la Posta Tanzania (TPC), wakati ulipomtembelea ofisini kwake kwa kumueleza mafanikio na changamoto mbalimbali zinzolikabili shirika hilo, Dar es Salaam leo. Wa pili kulia ni Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania (TPC), Deo Kwiyukwa, kushoto ni Maofisa Waandamizi kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Joseph Mwaisemba na Mathias Shabaha na kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu Rasilimali za shirika, Macrice Mbodo.(Picha zote Joseph Ngowi wa TPC)


UONGOZI wa Shirika la Posta Tanzania (TPC), leo umefanya ziara ofisini kwa Msajili wa Hazina Dkt. Oswald Mashindano na kufanya mazungumzo nae. Huu ni mwendelezo wa mikakati na juhudi za uongozi mpya wa Shirika wa kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazolikabili shirika la Posta.

Ujumbe huo wa Shirika la Posta uliongozwa na Kaimu Postamasta Mkuu, Bw. Deogratius Kwiyukwa,Kaimu Meneja Mkuu wa Rasilimali za shirika, Bw. Macrice Mbodo na ofisa wa mawasiliano wa shirika Bw. Joseph Ngowi.

Katika mazungumzo hayo, ujumbe kutoka Shirika la Posta ulimweleza Msajili hali halisi ya shirika, zikiwemo changamoto , mafanikio na maendeleo ambayo shirika limeyapata tangu lilipoanzishwa mwaka 1994 baada ya kutenganishwa na Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) na Benki ya Posta ambao kwa sasa ni taasisi zinazojitegemea kama ilivyo Shirika la Posta.
Postamasta Mkuu alieleza juu ya hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Shirika katika kulifanyia mabadiliko makubwa ya kimuundo na kiutendaji ili liweze kukabiliana na changomoto za ushindani wa huduma na biashara kwa jumla. Pamoja na mambo mengine alimwomba msajili wa hazina, alisaidie Shirika katika kutatua changamoto mbali mbali.

Baadhi ya changamoto alizozitaja katika mazungumzo hayo ni pamoja na:-

Shirika la Posta kuwekwa kwenye orodha ya Mashirika yanayotarajiwa kurekebishwa au kubinafsishwa hatua iliyolidhoofisha Shirika. pamoja kikwazo hicho Shirika la Posta linabeba mzigo mkubwa wa kuwalipa watumishi wake mishahara na marupurupu yao bila kuitegemea Serikali ikizingatiwa kwamba Shirika halikupewa mtaji na haliruhisiwa kukopa kwa ajili ya kujiendesha.

Alimkumbusha msajili juu ya dhamana ya serikali kuwa Shirika la Posta ni mali ya Serikali kwa asilimia mia moja (100%) na sheria namba 19 ya mwaka 1993 iliyoanzisha Shirika la Posta inatamka wazi kuwa Serikali kupitia hazina chini ya Waziri wa Fedha atakaa na Waziri mwemye dhamana ya Posta ili kubaini mtaji utakaowezesha Shirika kujiendesha, hadi sasa mtaji huo haujaweza kutolewa ili kuliwezesha Shirika kujiendesha.

Kaimu Postamasta Mkuu Bw. Kwiyukwa amemwomba Msajili wa Hazina kurejesha fedha kiasi cha shilingi 3,977,000,000/= ambazo Shirika lilizitumia kulipa Pensheni ya wastaafu wa lililokuwa Shirika la Posta na Simu la Jumuia ya Afrika Mashariki.

Vilevile alimuomba kuhamisha jukumu la kuwalipa wastaafu hao kwenye Mifuko ya hifadhi ya jamii. Serikali iangalie uwezekano wa kuchukua mzigo wa riba na tozo (Interest and Penalty) na malimbikizo ya kodi ya shilingi 29,000,833,757/= ambayo kati ya hizo, tozo na riba ni shilingi 22,013 701,414.28.

Bw. Kwiyukwa alimweleza Msajili wa Hazina kuwa haya yote yakifanyika kwa wakati Shirika litaweza kujiendesha kwa faida na kutoa gawio kwa mwenye mali (Serikali) kama ilivyokusudiwa.

Pia alieleza kuwa kwa sasa Shirika linafanya mabadiliko makubwa ya kimfumo na ya kimuundo ambapo linahitaji fedha kwa ajili ya kuboresha huduma zake, kuanzisha miradi mipya na kuimarisha zile zilizoko.

Mwisho, Dkt. Mashindano aliahidi kuyafanyia kazi maombi hayo kwa karibu na kuangalia namna ya kutatua changamoto hizo. Aliahidi pia kuyafanyia kazi mara moja yale yote yanayohusiana na ofisi ya hazina na yaliyoko chini ya uwezo wake, na yale mengine hatua kwa hatua ili shirika la Posta liweze kutoa huduma bora kwa wananchi, ili liweze kujiendesha kwa faida na hatimaye kuweza kutoa gawio kwa Serikali.




Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania (TPC), Deo Kwiyukwa (wa pili kulia), akimuelezea changamoto mbalimbali zilizolikabili shirika hilo, Msajili wa Hazina, Dkt. Oswald Mashindano (katikati), wakati uongozi wa TPC, ulipokutana naye na kufanya mazungumzo jijini Dar es Salaam leo. Wengine, kushoto ni Maofisa Waandamizi kutoka Ofisi yake, Joseph Mwaisemba na Mathias Shabaha na kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu Rasilimali za shirika, Macrice Mbodo.



Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania (TPC), Deo Kwiyukwa (wa pili kulia), akimuelezea changamoto mbalimbali zilizolikabili shirika hilo, Msajili wa Hazina, Dkt. Oswald Mashindano (kushoto), wakati wa ziara hiyo, Dar es Salaam leo. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu Rasilimali za shirika, Macrice Mbodo.



Msajili wa Hazina, Dkt. Oswald Mashindano (katikati), akiueleza jambo uongozi wa Shirika la Posta Tanzania (TPC), wakati ulipomtembelea ofisini kwake, Dar es Salaam leo. Katikati ni Kaimu Postamasta Mkuu, Deo Kwiyukwa na kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu Rasilimali za shirika, Macrice Mbodo.



Kaimu Mkurugenzi Mkuu Rasilimali za shirika, Macrice Mbodo (kulia), akifafanua jambo kwa Msajili wa Hazina, Dkt. Oswald Mashindano (kushoto), walipomtembelea ofisini kwake jijini leo.



Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania (TPC), Deo Kwiyukwa (wa pili kuli), akimonesha picha kwenye kompyuta za utakaokuwa muonekano mpya wa vyombo vya usafirishaji na Ofisi za shirika, Msajili wa Hazina, Dkt. Oswald Mashindano wakati wa ziara hiyo, jijini Dar es Salaam leo.



Msajili wa Hazina, Dkt. Oswald Mashindano na wasaidizi wake pamoja na uongozi wa Shirika la Posta, wakifurahia utakokuwa muonekano mpya vyombo vya usafirishaji na Ofisi za shirika.



Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania (TPC), Deo Kwiyukwa (katikati), akimonesha Msajili wa Hazina, Dkt. Oswald Mashindano picha ya moja ya gari kwenye kompyuta la usafirishaji barua na vifurushi vya wateja wa shirika.



No comments:

Post a Comment