Friday, August 11, 2017

TANDAHIMBA YAJIHIMARISHA KILIMO CHA KOROSHO, YAOMBA MAFUNZO ZAIDI


PICHANI: Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba Mkoani Mtwara, Sebastiana Waryuba, akifungua mafunzo kwa maofisa ugani wa wilaya hiyo leo yanayohusu jinsi ya kutumia sayansi na teknolojia katika kuboresha kilimo ambayo yaliandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kupitia Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB). Kutoka kulia ni Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmshauri hiyo katika ufunguzi ma mafunzo hayo, Diwani wa Kata ya Lukokoda, Chimale Abdallah na Ofisa Utumishi, Ahmada Suleimani.


Na Dotto Mwaibale, Tandahimba- Mtwara

WILAYA ya Tandahima Mkoa wa Mtwara imejihimarisha kwa kilimo cha zao la biashara la korosho na kuwa ya kwanza kwa kilimo cha zao hilo kitaifa ambapo kwa msimu wa mwaka 2016/2017 ilipata tani 68,399 ukilinganisha na msimu wa mwaka 2015/2016 ambapo walipata tani 47,000.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Sebastian Waryuba wakati akifungua mafunzo kwa maofisa ugani wa wilaya hiyo leo yanayohusu jinsi ya kutumia sayansi na teknolojia katika kuboresha kilimo ambayo yameandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kupitia Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB).

"Wilaya yetu inafanya vizuri katika kilimo lakini tunahitaji kufanya vizuri zaidi ya hapa na hapo ndipo tukapovivunia mafanikio yetu" alisema Waryuba.

Alisema katika kufanikisha jambo hilo kama viongozi wa serikali wana wajibu wa kuhakikisha malengo yaliyowekwa na serikali ya kuzalisha chakula kwa wingi yanafikiwa na malengo hayo yatawezekana tu iwapo maofisa ugani watakuwa na utaalamu juu ya matumizi ya bioteknolojia kwenye kilimo.
Waryuba ameiomba Tume ya Taifa ya sayansi na Teknolojia (COSTECH) kuendelea kuwapa mafunzo maofisa ugani wa wilayani kwake ya namna ya kutumia teknolojia kwenye kilimo ili waweze kuzalisha kwa wingi zao la muhogo na mahindi kama ilivyo kwenye korosho.

“Sisi Tandahimba tunahitaji kuzalisha kwa wingi zaidi muhugo na mahindi kama tunavyozalisha korosho, tupatieni utaalamu wa kutumia hizi bioteknolojia,” alisema Waryuba.

Mkuu huyo wa wilaya alisema kwamba wilaya yake ya Tandahimba ni wakulima hodari na hawana upungufu wa chakula wala njaa na hana wasiwasi kama Rais alivyosema kuwa iwapo njaa itatokea katika wilaya fulani basi mkuu wa wilaya na mkurugenzi itakuwa kwa heri. " Mimi nasema hapa kwetu hatuna njaa, sio kwamba nadanganya ndio ukweli wenyewe.”

Alitoa mwito kwa Costech kuhakikisha kwamba wanatoa machapisho ya kutosha kwa kila ofisa ugani wa kijiji na kata ili wawe wanasoma na kujikumbusha mafunzo hayo ili waweze kuyafuatilia kwa asilimia 100 na kuyatekeleza kwa asilimia 100.

“Maofisa ugani kupatiwa mafunzo ya kutumia teknolojia kwenye kilimo ni jambo la msingi kwani watasaidia uzalishaji wa mazao kuongezeka hivyo kupata chakula na kuondoa njaa kwa wananchi,” alisema.

Alisema Muhogo na Mahindi ni mazao yanayotakiwa kuzalishwa kwa njia bora zaidi ili wilaya hiyo iweze kuwa na ujasiri wa kutafuta wawekezaji wa viwanda kutoka nje kuja kuwekeza wilayani hapai. Alisema mafunzo haya ni mchakato wa kuandaa watalamu watakaosadia kupatikana kwa malighafi za viwandani.

Alisema pamoja na mafanikio hayo, lakini wilaya yake inakabiliwa na changamoto za ukosefu wa skimu za umwagiliaji pamoja na masuala ya ushirika.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba, Ahmada Suleimani alisema Mihogo ya Tandahimba inasoko katika nchi za Sudan Kusini na China, lakini changamoto ni mazao yenyewe kuzalishwa kidogo na hivyo kutotosheleza mahitaji ya wateja hao kutokana na kulima kwa njia ya kizamani na kupata tija kidogo.

“Ukweli ni kwamba tunahitaji elimu kubwa kwa ajili ya kuzalisha muhogo kwa wingi na tunaamini kwamba semina hii itasaidia maofisa wetu wa ugani wa vijiji na kata waweze kuwa na elimu ya kuwasaidia wakulima wetu waweze kuzalisha kwa wingi mazao hayo,” alisema Suleimani.

Mafunzo yanayotolewa na Costech yamelenga matumizi ya bioteknolojia kwa mazao kama mahindi, muhogo na koroshao ambapo mafunzo hayo mbali ya kutolewa kwa maofisa ugani na wakulima wa mkoa wa Lindi kwa mkoa wa Mtwara yameanza jana kufanyika katika Halmshauri ya Wilaya ya Mtwara na Manispaa ambapo kesho yataendelea katika Halmshauri ya Wilaya ya Newala.


(Imeandaliwa na mtandao wa www.habari za jamii.com-simu namba 0712727062)








Ofisa Utumishi, Ahmada Suleimani, akimkarisha mkuu wa wilaya kufungua mafunzo hayo.



Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmshauri hiyo katika ufunguzi ma mafunzo hayo, Diwani wa Kata ya Lukokoda, akizungumza kabla ya kufungua mafunzo hayo. Kutoka kushoto ni Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Wilaya hiyo, Domina Soko, Mwenyekiti wa CCM Wilaya, Abdul Namtula, Mkuu wa Wilaya, Sebastian Waryuba na Ofisa Utumishi, Ahmada Suleimani.




Mtafiti kutoka COSTECH, Bestina Daniel, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Costech kuhusu mafunzo hayo na umuhimu wake katika kilimo. Kulia ni Mshauri wa Kilimo na Ushirika Mkoa wa Mtwara, Ally Linjenje.




Mwezeshaji kutoka OFAB, Dk. Emmarold Mneney, akitoa mada kuhusu matumizi ya Sayansi na Bioteknolojia katika kilimo cha kisasa.




Ofisa Ugani kutoka Kata ya Chingungwe, Sizya Lugembe, akiuliza swali kuhusu dhana potofu juu ya matumizi ya bioteknolojia katika kilimo.




Mtafiti wa Mazao ya Mizizi na Jamii ya Viazi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo, Naliendele Mtwara, Benadetha Kimata, akitoa mada kuhusu kilimo cha mihogo bora.



Ofisa Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika wa wilaya hiyo, Issa Naumanga, akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.




Maofisa ugani wakiwa katika mafunzo.

Mshauri wa Jukwaa la Matumizi ya Bioteknolojia ya kisasa katika kilimo, Dk.Nicholaus Nyange, akitoa mada kuhusu kilimo cha mahindi yanayostahimili ukame.




Mafunzo yakiendelea.




Usikivu katika mafunzo hayo.




Maofisa ugani wakiwa makini kuandika kila kilichokuwa kikifundishwa.




Taswira ya ukumbi wa mafunzo.




Viongozi wakihudhuria mafunzo hayo.




Jengo la Ukumbi wa Mikutano la Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba.





No comments:

Post a Comment