PICHANI: Meneja Mkaazi wa Kampuni ya Jumia Travel Tanzania, Fatema Dharsee, akizungumza katika hafla fupi ya uwasilishwaji wa Ripoti ya Utalii Tanzania kwa mwaka 2017 kutoka katika kampuni hiyo inayojishughulisha na huduma za hoteli na usafiri mtandaoni tukio lililofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip katikati ya jiji la Dar es Salaam leo asubuhi.
Na Dotto Mwaibale
SERIKALI imeahidi kuendelea kuwashirikisha
wadau mbalimbali katika sekta ya utalii hususani kwenye utungaji wa sera
pamoja na kutengeneza mazingira mazuri ya uendeshwaji wa shughuli hizo
nchini Tanzania.
Hayo yalisemwa na Ofisa Habari na Mawasiliano wa
Shirikisho la Utalii Tanzania, Denis Simkoko katika hafla fupi ya
uwasilishwaji wa Ripoti ya Utalii Tanzania kwa mwaka 2017 kutoka kwa
Jumia Travel, kampuni inayojishughulisha na huduma za hoteli na usafiri
mtandaoni tukio lililofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Golden Tulip
katikati ya jiji la Dar es Salaam leo asubuhi.
“Bila shaka
mafanikio tuliyonayo kwa sasa katika sekta ya Utalii nchini ni matokeo
mazuri ya ushirikiano wa karibu baina ya serikali na wadau wengine.
Shirikisho la Utalii Tanzania lipo kama daraja katika kuwaunganisha
wadau mbalimbali wa sekta hii nchini kote na wizara husika yenye mamlaka
kwa mujibu wa serikali. Huwa tunakutana na wadau wa utalii ambapo ni
takribani vyama 12 nchini kote ndani ya kipindi maalumu cha mwaka na
kujadili masuala mbalimbali yanayotukabili. Baada ya hapo sasa ndiyo
sisi kama shirikisho huwa tunayawasilisha maoni hayo kwa serikali ili
kupata ufumbuzi na pia kutengeneza fursa ambazo zitatukutanisha pamoja
wadau katika meza moja ya majadiliano, “ alisema Simkoko.
“Mbali
na mchango wetu kwenye kupendekeza maboresho ya kodi na sera, pia tunao
watu wetu kwenye vikosi kazi na kamati mbalimbali ambao hufanya kazi
kwa ukaribu na serikali. Ingawa bado kuna changamoto katika kupata
ushirikiano kamili au wa moja kwa moja baina ya serikali na sekta
binafsi, bado tunaimani juu ya mifumo thabiti na ya uwazi katika
uandaaji na ufanyikaji wa mikutano, majadiliano na mafunzo. Kwa
kuongezea pia tunahamasisha uboreshwaji wa nyanja mbalimbali katika
utolewaji wa huduma na sekta binafsi kama vile kuwekeza kwenye
rasilimali watu. Kwa kushirikiana na taasisi tofauti kama vile
Shirikisho la Wamiliki wa Hoteli Tanzania na Chuo cha Utalii cha Taifa
tunatoa mafunzo kwa vijana kwa kuwapatia ujuzi ili waweze kuajirika kwa
urahisi kwenye sekta hii nchini,” alimalizia Afisa Habari na Mawasiliano
wa kutoka Shirikisho la Utalii Tanzania.
Meneja Mkaazi wa Jumia
Travel Tanzania, Fatema Dharsee amebainisha kuwa maendeleo ya sayansi na
teknolojia hususani kuongezeka kwa watumiaji na ueneaji wa mtandao wa
intaneti umechochea kwa kiasi kikubwa kukua kwa sekta ya utalii nchini.
“Tanzania
mpaka hivi sasa ina watumiaji wa intaneti zaidi ya milioni 19 kufikia
mwaka 2016 kutoka milioni 17 mwaka 2015. Hilo ni sawa na ongezeko la
asilimia 0.9 kwa mwaka na ueneaji wa mtandao wa intaneti wa asilimia 83
miongoni mwa watanzania milioni 50 nchi nzima. Hii ni ishara nzuri kwetu
sisi Jumia Travel ukizingatia kwamba jitihada zetu kubwa ni kuhakikisha
kuwa tunawawezesha watanzania kufanya huduma za hoteli na usafiri kwa
njia ya mtandao. Katika ripoti yetu tuliyoiwasilisha inaonyesha kwamba
idadi kubwa ya wateja wanaotafuta huduma kupitia mtandaoni inazidi
kuongezeka kitu ambacho ni kizuri kwenye sekta ya utalii,” alisema
Dharsee.
“Kupitia ripoti hii tumebaini kwamba idadi kubwa ya
watanzania kwa sasa wanatumia simu za mkononi (asilimia 60) kutafuta
hoteli mitandaoni ukilinganisha na kompyuta (asilimia 40). Lakini cha
kuvutia zaidi kwenye upande wa kufanya huduma hupendelea zaidi kompyuta
(asilimia 65) badala ya simu za mkononi (asilimia 35). Idadi kubwa ya
hoteli zinazotafutwa na kutumiwa zaidi na wateja ni za nyota mbili
(asilimia 41) na tatu (asilimia 39) ambapo bado zile za nyota moja na
tano zikionyesha kutembelewa na wateja wachache kwa vigezo vya huduma
hafifu (kwa zile za nyota moja - asilimia 4) na gharama kubwa (kwa zile
za nyota tano - asilimia 4),” aliongezea Dharsee.
Meneja Mkaazi
huyo wa Jumia Travel nchini alihitimisha kwa kufafanua juhudi
wanazozifanya katika kuwawezesha wamiliki wa hoteli na wateja kuendana
na mabadiliko ya teknolojia kwenye utoaji wa huduma. Ambapo kwa kiasi
kikubwa karibuni kila pembe ya dunia watoa huduma na wateja wamehamia
mtandaoni kwani kuna urahisi na unafuu mkubwa kwa pande zote mbili.
“Tunafanya
juhudi kubwa katika kuwahamasisha wamiliki au mameneja wa hoteli pamoja
na wateja kutumia zaidi huduma kwa njia ya mtandao kwani ni rahisi,
gharama nafuu na ya uhakika. Kwa upande wa mahoteli tunawasaidia kwa
kiasi kikubwa kuwatangaza kwa maelfu ya wateja tulionao nchini pamoja na
kuwapatia mfumo rahisi wa kuendesha shughuli zao. Kwa mfano, mteja
kupitia mtandao wetu amerahisishiwa kwa kupunguziwa ile adha ya
kutembelea hoteli moja baada ya nyingine kwenye kutafuta ile itakayomfaa
zaidi,” alihitimisha Dharsee.
Meneja Uhusiano wa kampuni hiyo, Geofrey Kijangwa akizungumza kwenye hafla hiyo.
Uzinduzi ukiendelea.
Ofisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Utalii Tanzania, Denis Simkoko akizungumza katika hafla hiyo.
Maofisa wa Shirikisho la Utalii Tanzania (TCT), wakiwa kwenye hafla hiyo. Kutoka kulia ni Ofisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho hilo, Denis Simkoko, Meneja Mkuu wa Mauzo wa Hoteli ya Ramada Resort Dar es Salaam, Amina Kapya na Ofisa Tawala wa Chama cha Wamiliki wa Hoteli Tanzania (HAT), Jeniffer Abel.
(Imeandaliwa na mtandao wa www.habari za jamii.com-simu namba 0712727062)
No comments:
Post a Comment