Tuesday, November 15, 2016

TANESCO YAAHIDI UMEME WA UHAKIKA KATIKA TANZANIA YA VIWANDA


Ziara ya hivi karibuni ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Felchesmi Mramba, alipotembelea kituo kipya cha kupoza na kusambaza umeme cha Ilala Mchikichini jijini Dar es Salaam


NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID

KUONGEZEKA kwa shughuli za Kiuchumi pamoja na ongezeko la idadi ya Watu waliopatiwa Huduma ya umeme Nchini, kumefanya mahitaji ya umeme kuwa makubwa zaidi. Mathalan takwimu zinaonesha, mahitaji ya juu ya umeme yameongezeka kutoka MW 988.27 Mwezi Desemba 2015 hadi kufikia MW 1,026.02 Mwezi Machi, 2016 sawa na ongezeko la asilimia 4.

Wizara ya Nishati na Madini kupitia Shirika la Umeme Nchini Tanzania (TANESCO), imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuboresha Miundombinu ya umeme kote Nchini ili Wananchi waweze kupata umeme ulio bora na wa uhakika zaidi na hivyo kuemdana na malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano ambayo imedhamiria kujenga uchumi wa Viwanda.

Miongoni mwa hatua ambazo TANESCO imekuwa ikichukua ni pamoja na kukarabati na kubadilisha Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji umeme kwenye maeneo kadhaa ya Nchi.

Hali ya upatikanaji umeme Nchini kwa sasa imeendelea kuimarika siku hadi siku ukiachilia mbali katika baadhi ya maeneo Nchini ambayo umeme hukosekana kwa sababu ya hitilafu za muda mfupi pamoja na matengenezo yanayoendelea hivi sasa kote nchini ya kukarabati na kubadilisha Miundombinu ya umeme.

Kwa sasa uwezo wa mitambo ya kufua umeme (installed capacity) Nchini ni MW 1,439.97 ambapo MW 1357.69 ni mitambo iliyounganishwa katika Gridi ya Taifa na kiasi cha MW 82.28 ni mitambo iliyo nje ya Gridi (Isolated stations).Uwezo wa mitambo ya kufua umeme katika Gridi ya Taifa kwa kutumia nguvu za maji (hydropower) ni MW 566.79 sawa na asilimia 41.70 ya mitambo yote. Mitambo itumiayo Gesi Asilia ni MW 607.00 sawa na asilimia 44.7 wakati Mitambo ya kufua umeme kwa kutumia mafuta ina uwezo wa MW 173.40 sawa na asilimia 12.8, na umeme unaofuliwa kwa kutumia biomass ni MW 10.5 sawa na asilimia 0.8 ya mitambo yote.


Katika kuhakikisha hali ya upatikanaji umeme Nchini itakayokwenda sambamba na malengo ya Serikali ya kujenga Uchumi wa Viwanda inaimarika zaidi, Wizara kupitia TANESCO imekuwa ikitekeleza sio tu Miradi ya Ufuaji umeme bali pia miradi ya njia za Usafirishaji na Usambazaji umeme.

Utekelezaji wa miradi hii uko katika hatua mbili za muda mfupi na muda mrefu ambapo baadhi ya Miradi tayari imekamilika na mingine iko katika hatua mbalimbali. Miradi ambayo kwa asilimia kubwa tayari imekamilika ni pamoja na ile ya kuimarisha Miundombinu ya Kusambaza na Kusafirisha umeme katika Majiji na Miji hapa Nchini, ambayo ni;

Mradi wa kuimarisha upatikanaji wa umeme katika Jiji la Dar es Salaam ambapo ujenzi wa kituo cha Kupoza umeme katikati ya Jiji upo katika hatua za mwisho za kukamimilika (Improving the Electricity Power Supply relability in City of Dar es Salaam), ambapo mradi huu unafadhaliwa na Serikali ya Finland pamoja na Serikali ya Tanzania.

Mradi mwingine ni ule wa Tanzania Energy Development and Access Project (TEDAP) unatekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Kilimanjaro. Mradi unakusudia kuboresha na kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika mikoa husika . Mradi huu unahusisha ujenzi wa miundombinu ya kusambaza, kusafirisha pamoja na vituo vya kupoza umeme.

Mradi wa uzalishaji umeme uliokamilika ni ule wa ujenzi wa mitambo ya Kinyerezi I (MW 150) Mwezi Machi, 2016 na katika kipindi cha Mwaka 2016/17 ujenzi wa mitambo mipya ya Kinyerezi I Extension (MW 185) na Kinyerezi II (MW 240) umeanza kutekelezwa.

Utekelezaji wa ujenzi wa miradi hii ya uzalishaji umeme umekuwa ukienda sambamba na utekelezaji wa ujenzi wa miradi ya njia za kusafirisha na kusambaza umeme, kama ule wa kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Iringa hadi Shinyanga (backborne) ambapo upo katika hatua za mwisho kukamilika.


Mradi huu wa backborne utaimarisha upatikanaji wa umeme katika maeneo ya Kanda ya Ziwa, Kati na Kaskazini. Mradi huu umekamilika kwa asilimia 98 hadi hivi sasa.


Pia kuna Mradi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Makambako hadi Songea wa msongo wa kilovoti wa 220 wenye urefu wa kilomita 250 pamoja na kusambaza umeme katika mikoa ya Njombe na Ruvuma. Kazi zinazoendelea ni ujenzi wa miundombinu ya kusambaza umeme.


kwa upande wa njia ya kusafirisha umeme, kazi zinazoendelea ni usanifu wa kina (Detail Feasibility Study), uingizwaji wa vifaa vya ujenzi na uandaaji wa eneo la mradi (Site Moblization).






Lakini pia TANESCO inatekeleza miradi mwingine wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 yenye urefu wa kilomita 1,148 kutoka Mbeya - Sumbawanga- Kigoma - Nyakanazi (North - West Transmission Line);






Kwa upande wa Kaskazini mwa nchi yetu TANESCO inatekeleza Mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 yenye urefu wa kilomita 664 kutoka Dar es Salaam - Chalinze – Tanga - Arusha (North - East Transmission Line). Kazi zinazoendelea kwa sasa ni kuweka mipaka kwenye njia ya kusafirisha umeme;






Mradi mwingine ni wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Somanga fungu hadi Dar es Salaam (Kinyerezi), gharama za mradi ni Dola za Marekani milioni 150. Kwa sasa Serikali inatafuta fedha za kutekeleza mradi husika;


Sekta binafsi nayo haikuachwa nyuma katika harakati za uzalishaji na usafirishaji umeme nchini.


Kwa kuzingatia kuwa azma ya Serikalini kufikia uzalishaji wa umeme wa Megawati 5,000 ifikapo 2020 na Megawati 10,000 ifikapo 2025. Serikali ilianzisha mkakati maalum wa kuongeza uwekezaji katika miradi ya kuzalisha umeme ambayo inatekelezwa kwa kushirikiana na sekta binafsi kutoka ndani na nje ya nchi.






Kwa upande wa miradi ya uzalishaji umeme, sekta binafsi imeshirikishwa katika miradi midogo ya Nishati Jadidifu (Renewable Energy) yenye MW 16.29 imetekelezwa na sekta binafsi, nayo ni Miradi midogo ya kuzalisha umeme wa maji (Min Hydropower) ambayo ni Uwemba- MW 0.84; Mwenga MW 4; na Yori MW 0.95; na Miradi midogo ya kuzalisha umeme kwa kutumia tungamo taka (Biomass) ni Tanwat MW 1.5 na TPC MW 9.0.





Kilwa Energy Gas Fired Plant (371.2 MW)- US$ Milioni 465, Mwekezaji yupo katika hatua za mwisho za majadiliano ya Mikataba mbali mbali ambayo ni; Mkataba wa nyongeza wa utekelezaji (Addendum to Implementation Agreement), Mkataba wa Ubia (Shareholders Agreement), na Mkataba wa kununua gesi asilia (Direct Gas supply Agreement) ili kupata ufadhali wa mradi.


Kwa upande wa Miradi ya usafirishaji umeme, uwekezaji kwenye miundombinu ya usafirishaji wa umeme ni jukumu la Serikali na si sekta binafsi. Aidha, Sheria ya umeme ya Mwaka 2008 inaruhusu sekta binafsi kupitisha umeme kwenye miundombinu hiyo kwa kulipia Wheeling Charge na wala si kumiliki miundombinu husika.


Hatua hizi za Wizara ya Nishati na Madini kupitia TANESCO hazikuishia kuboresha upatikanaji umemem mijini tu bali pia vijijini, ambapo kupitia mpango wa kusambaza umeme vijijini REA ambapo sasa mpango huo uko katika awamu ya tatu (REAIII). Miradi mbalimbali inatekelezwa ikiwa ni pamoja na kukamilika kwa mradi wa Turnkey Phase II.






Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Pili umekamilika kwa asilimia 92.5%. Ambapo, wateja 110,868 kati ya 257, 000 wameunganishiwa umeme sawa na asilimia 43%;


Wilaya mpya 13 zimepatiwa umeme: Busega, Buhigwe, Chemba, Itilima, Kakonko, Kalambo, Kyerwa, Mkalama, Mlele, Momba, Nanyumbu, Nyasa na Uvinza;


Lakini pia Mradi kabambe wa kupeleka umeme Vijijini (REA Turnkey Phase III) unaotekelezwa katika kipindi cha miaka mitano (5) kuanzia 2016-2020, inategemewa vijiji vyote hapa nchini vitapata huduma ya umeme baada ya kukamilika kwa mradi huu.






Mpaka sasa upatikanaji wa Huduma ya umeme (electricity access level) kitaifa umekua na kufikia asilimia 40, ambapo Wananchi waliounganishwa na Huduma ya umeme (electricity connection level) ni asilimia 36 (Juni, 2016).






Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA TURNKEY PHASE III).


Mradi huu utatekelezwa kwa kipindi cha miaka 5 katika vijiji 7,873 vya wilaya zote za Tanzania Bara. Takribani Vijiji 7,697 vitapelekewa umeme wa Gridi ya Taifa na Vijiji 176 umeme wa nje ya Gridi (Off-grid).


Mpango huu utaongeza wigo wa Usambazaji umeme katika maeneo ambayo hayakufikiwa na Mradi wa REA Turnkey Phase II. Wakandarasi watakaojenga Miundombinu ya Mradi huu wameshapatikana. Shilingi Bilioni 587.61 zimetengwa kutekeleza Mradi huu katika kipindi cha Mwaka 2016/17. Kati ya fedha hizo Shilingi bilioni 534.40 ni fedha za ndani na Shilingi Bilioni 53.21 ni fedha za nje.


Serikali kupitia TANESCO pia inaendelea kuhimiza Wananchi kuunganisha Huduma ya umeme katika maeneo yao ya Vijijini hii ni baada ya utekelezaji wa Miradi Kabambe ya REA kufanikiwa kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na kasi ya Wananchi ya kuunganisha Huduma ya umeme.


















No comments:

Post a Comment