Wednesday, October 19, 2016

DC HAI AMALIZA MGOGORO WA ARDHI, AREJESHA SHAMBA KWA HALMASHAURI YA WILAYA YA HAI

Mkuu wa wilaya ya Hai,Gelasius Byakanwa akizungumza wakati wa mkutano wa hadhara na wananchi wa vijiji vinne vilivyoko kata ya Machame Narumu akitoa uamuzi juu ya mgogoro wa ardhi wa shamba la Fofo estate.

Baadhi ya Wananchi waliofika katia Mkutano huo.

Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii Kanda ya Kaskazini.

MGOGORO wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miaka 40 wa shamba la Fofo lilipo wilayani Hai ,umemalizika baada ya Mkuu wa wilaya hiyo ,Gelasius Byakanwa kutangaza kurejesha shamba hilo chini ya usimamizi wa Halmashauri ya wilaya ya Hai.

Hatua ya Mkuu huyo wa wilaya inatokana na mgogoro baina ya Wananchi wa vijiji vinne vya Urori,Tella ,Mula na Usali vilivyoko kata ya Machame Narumu lilipo Shamba hilo dhidi ya aliyekuwa mtendaji mkuu wa Chama cha Ushirika cha Narumu Manushi,Peter Karanti anayedaiwa kujimilikisha shamba hilo .

Akitoa historia ya mgogoro huo Byakanwa alisema shamba hilo lililopewa namba 240 na 242 Ex .C.T No.NP 405 EP.LOT.661 (FOFO ESTATE) lilikuwa linamilikiwa na raia wa kigeni Dkt A Phones ambaye aliweka rehani shamba hilo mwaka 1966 kwa ajili ya mkopo wa kiasi cha Sh 100,000 kutoka benki ya CRDB .

“Baadae Dkt ,Phoneas alitoroka nchini kabla ya kulipa mkopo huo ,Benki baada ya kugundua hilo ilichukua hatua ya kuliza shamba ili kurudisha mkopo aliokuwa akidaiwa Dkt Phoneas”alisema Byakanwa.

Alisema Chama cha Ushirika cha Narumu Manushi ambacho wanachaa wake ni wananchi wa vijiji vine lilipo shamba hilo kilifanikiwa kununua shamba hilo kwa kulipia deni la sh 100,000 ambapo kilitoa kiasi cha Sh 20,000 huku kikibaki na deni la sh 80,000.

“Taarifa ambazo ofisi yangu ilizipata ni kuwa chama kilipewa miaka 10 kiwe kimemaliza kulipia deni hilo ,lakini ndani ya miaka miwili zikatokea taarifa za kuwa Chama cha Ushirika cha Narumu kilishindwa kumaliza deni lake”alisema Byakanwa.

“Bahati mbaya zaidi ,shahidi wa taarifa hizi ni Peter Karanti aliyekuwa mtendaji mkuu wa chama cha Ushirika na haikujulikana yeye kama mtendaji mkuu alichukua hatua gani za kuhakikisha chama kinamaliza deni lake”aliongeza Byakanwa.

Alisema hakuna ushahidi unaoonesha kuwa benki ya CRDB ilikususdia kuliuza shmaba hilo kwa kigezo cha kuwa Chama cha Ushieika cha Narumu kimeshindwa kulipa deni ndani ya muda husika zaidi ya kuwepo kwa taarifa kuwa Mtendaji mkuu wa Chama cha Ushirika alitafuta baadhi ya wanachama na wasio wanachama wachange pesa ya kulikomboa na kulimiliki.

“Baadae chama cha ushirika kilipitisha maamuzi ya kuwapa jukumu la kulipa deni la chama,Karanti na wenzake walilipa deni na kukabidhiwa Shamba hata hivyo walishindwa kupata hati miliki ya Shamba hilo kwa kuwa ilikua bado inashikiliwa na benki kutokana na mkataba uliokuwepo ulikuwa ni Chama cha Ushirika na si Karanti na wenzake.

Akitoa maamuzi juu ya mgogoro huo wakati wa mkutano wa hadhara na wananchi wa vijiji hivyo uliofanyika katika uwanja wa michezo wa shule ya sekondari Tunoma ,Byakanwa alitangaza kuzuia kufanyika kwa shughuli za maendeleo katika shamba la Fofo zinazofanywa na mtu binafsi.

“Kwa kuwa hati ya Dkt Phoneas aliyekuwa mmiliki wa shamba hilo ilikwisha batilishwa na kuamuliwa shamba hilo limilikishwe kwa kijiji na vijiji ndivyo vinalipa kodi ya ardhi,wakulima wote waliolima katika shmba hilo wavune mazao yao ndani ya kipindi cha miezi mitatu” alisema Byakanwa.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ya ufuatiliaji wa shamba hilo John Kweka alisema awali Wenyeviti wa vijiji hivyo ndio walikuwa wakifuatilia mgogoro huo kabla ya kubaini kuwa wenyeviti hao kuwa na maslahi katika mgogoro na kulazimika kuunda kamati nyingine.

“Tumefuatilia hili suala hadi kwa Waziri wa Ardhi,tumepokea kwa furaha maamuzi ya mkuu wetu wa wilaya kwa sababu sisi kama kamati tulipendekeza maeneo katika hili shamba yatumike kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati,Shule ,Taasisi,Soko na Mahali pa kuzikia hili ndio lilikuwa lengo letu”alisema Kweka.
Mkuu wa wilaya ya Hai,Gelasius Byakanwa (aliyenyoosha mikono) akitoa ufafanzi wa jambo mara baada ya kutangaza kurejesha eneo lenye mgogoro kwa Halmashauri ya wilaya ya Hai.

Baadhi ya wananchi wa vijiji vinne vya Urori,Tella ,Mula na Usali waliohudhria mkutano wa Mkuu wa wilaya ya Hai wa kutoa maamuzi juu ya mggoro wa shamba la Fofo estate.

Baadhi ya wananchi wakiwa katika mkutano wa hadhara na Mkuu wa wilaya ya Hai,Gelasius Byakanwa wakati akitoa uamuzi juu ya mgogoro wa Shamba hilo.



Shamba la Ekari 106 la FOFO ESTATE lililopo wilayni Hai ambao limekuwa na mgogoro kwa zaidi ya miaka 40.











No comments:

Post a Comment