Na Dixon Busagaga wa Michuzi Blog aliyeko Kigoma.
SHIRIKA la Hifadhi za Taifa (TANAPA) limetoa Sh. Milioni 584 kwa ajili ya ujenzi wa madaraja mawili ikiwa ni njia moja ya kutatua changamoto ya miundombinu ya barabara katika vijiji vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa Milima ya Mahale vilivyopo wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.
Baadhi ya wananchi wanaoishi katika vijiji vya Lukoma na Igalula wanakabiliwa na changamoto ya barabara jambo linalowafanya washindwe kufanya shughuli zao za kimaendeleo.
Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea vijiji hivyo vilivyoko mwambao mwa zimwa Tanganyika ,Mkuu wa idara ya ujirani mwema ,Mhifadhi Romanus Mkonda aliyataja madaraja hayo kuwa Lagosa na Lukoma.
“Daraja la Lagosa linatumia Sh. Milioni 296 wakati lile la Lukoma litatumia Sh. Milioni 288,” alisema. Alisema lengo la TANAPA ni kusaidia jitihada za serikali za kuimarisha mawasiliano ya barabara katika ukanda huo kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kiuchumi.
“Iwapo barabara hiyo itapitika itarahisisha usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa ukanda huu na pia Hifadhi yetu itaweza kupata watalii wengi kwa sababu usafiri uliopo sasa hivi ni wa maji na Ndege pekee,” alisema. Hata hivyo, alisema iwapo miundombinu hiyo ya barabara itakamilika itaepusha gharama kubwa ambazo Hifadhi inaingia kwa ajili ya kwenda mjini kununua vitu mbalimbali vya hifadhini.
Aliongeza kuwa barabara hiyo itawasaidia wananchi hao kupata huduma mbalimbali zinazopatikana nje ya eneo lao ikiwa ni pamoja na kusafirisha mazao na kuyapeleka masoko ya nje. “Kwa mfano tunapotaka kwenda mjini tunatumia Boti ambalo linatumia Lita 1000 za petroli kwenda na kurudi na oil lita 40...hivyo iwapo barabara zitakamilika gharama hizi zitapungua,” alisema.
Pia, alisema barabara hizo zikikamilika utalii utaongezeka na kuliongezea taifa pato. Aliongeza kuwa kwa mwaka wa fedha 2016/17, TANAPA imetenga Sh. Milioni 500 kwa ajili ya kujenga madaraja ya Nkonkwa na Igalula yaliyopo vijijini hapo.
Naye mwenyekiti wa kijiji cha Igalula, Mussa Matililo alisema iwapo madaraja hao yatakamilika itawarahisishia wananchi wa maeneo hayo katika shughuli zao za kilimo. “Pia, itarahisisha mawasiliano ya kijiji kimoja kwenda kijiji kingine kwa sababu kwa sasa mawasiliano yamekuwa magumu kutokana nah ii mito miwili,” alisema.
No comments:
Post a Comment