Serikali imeanza majadiliano na kampuni ya TING katika
kuboresha mapato ya uwanja wa Taifa kupitia matangazo uwanjani hapo.
Akizungumza hapo jana wakati wa kikao kati ya Wizara ya
Habari Utamaduni Sanaa na Michezo na kampuni hiyo, Kaimu Mkurugenzi Idara
ya Maendeleo ya Michezo Bw. Alex Nkenyenge amesema kuwa Serikali imefarijika
kupata maombi hayo kutoka kampuni ya TING ya kuboresha mapato ya uwanja wa
Taifa kupitia matangazo ambayo yatawekwa katika maeneo ya uwanja huo.
“Ndugu zetu TING wamekuja na wazo zuri sana na tumelipokea
na tunaahidi kuliangalia kwa jicho la tatu kwani ni fursa ya pekee kwetu, sio
kuboresha mapato tu bali kutangaza uwanja wetu na kuendeleza michezo kwa
ujumla” alisema Bw. Nkenyenge.
Aliongeza kuwa ni wakati sasa wa Serikali pamoja na Wananchi
kufaidika na uwanja wao ambao ni wa kipekee katika Ukanda wa Afrika Mashariki
na Kati kwani fursa hiyo itasaidia pia kuendeleza Kijiji cha Michezo Changamani
ambao pia ni mpango wa Serikali katika kuendeleza sekta ya michezo nchini.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu kutoka TING Mch. Dkt.
Veron Fernandos amesema kuwa kampuni yake itatoa ushirikiano kwa Serikali
kupitia Wizara na ni azma yao kuona wananchi wanaona faida ya kuwa na uwanja wa
kisasa ambao utawaletea mafanikio katika maendeleo ya michezo nchini.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi wa
Ndani wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bi. Esther Yonael
ameipongeza kampuni ya TING kwa kuona fursa na kuitumia kwani kuna kampuni
nyingi zinaweza kuwa ziliona hiyo fursa hii lakini sikakosa uthubutu wa kuleta
maombi Wizarani kushirikiana katika suala hilo ambalo linafaida kwa pande zote
mbili.
Aidha, Mkuu wa Masoko kutoka TING Bi. Bernice Hannah
ameihakikishia Serikali kuwa wamejipanga vizuri na wamefanya utafiti wa kina wa
mradi huo na kuona kuwa unawezeka ukafanyika na kuleta mabadiliko katika sekta
ya michezo nchini.
Kampuni ya TING imedhamiria kushirikiana na Serikali katika
kuboresha mapato ya uwanja wa Taifa na imejipanga kuwekeza Shilingi Billioni
moja kwa miaka minne katika miundombinu na wataalam.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi kutoka Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bw. william Challe akichangia hoja katika kikao baina ya Serikali na kampuni ya TING kushirikiana katika kuboresha mapato ya Uwanja wa taifa kupitia matangazo.
Mkuu wa Masoko kutoka TING Bi. Bernice Hannah akionesha jinsi kampuni yake itakavyoweka miundombinu ya kuweka matangazo ndani ya uwanja wa taifa katika kikao baina ya Serikali na kampuni ya TING kushirikiana katika kuboresha mapato ya Uwanja wa taifa kupitia matangazo.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani kutoka Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bi. Esther Yonael kichangia hoja akichangia hoja katika kikao baina ya Serikali na kampuni ya TING kushirikiana katika kuboresha mapato ya Uwanja wa taifa kupitia matangazo.
Baadhi ya maafisa wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na
Michezo wakifatilia kikao baina ya Serikali na kampuni ya TING kushirikiana
katika kuboresha mapato ya Uwanja wa taifa kupitia matangazo. (Picha
na Raymond Mushumbusi WHUSM)
No comments:
Post a Comment