Friday, June 24, 2016

KIJANA WA MUHEZA AFYEKA SEHEMU ZAKE ZA SIRI NA KORODANI

Na Mwandishi Wetu,
Muheza, Tanga
Kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la Festo Hozza (18) mkazi wa Amani Wilayani muheza amediriki kujikata sehemu zake za siri na korodani kwa kutumia kitu chenye makali mfano wa kisu na kuziondoa kabisa jambo lililowashangaza wakazi wa wilaya hiyo.

Awali akithibitisha kumpokea kijana huyo aliyekuwa katika hali mbaya Daktari wa idara ya upasuaji katika Hospitali ya Teule iliyopo Wilayani humo, Abasi Mussa alisema siku ya tarehe 14 mwezi juni walipokea mgonjwa aliyeletwa kwa ajili ya kushonwa mara baada ya kumkagua waligundua ameondoa sehemu zake za siri zote.

Dokta Abasi alisema mara baada ya kuchukua maelezo ya mwanzo kwa mgonjwa huyo alijieleza kuwa yeye mwenyewe ana tatizo la akili na alihisi alijiwa na vitu asivyovielewa kama mashetani ambavyo vilimuamuru kuondoa sehemu zake za siri.

Alisema kwa uchunguzi wa awali walioufanya walibaini kijana huyo alijikata na kitu chenye makali mfano wa kisu ambacho alitumia kujiondoa sehemu zake za siri ikiwemo uume pamoja na korodani zake kwa pamoja.
Alisema kijana huyo alipelekwa akivuja damu nyingi kutokana na jeraha kubwa alilokuwa nalo alipelekwa katika chumba kikubwa cha upasuaji kwa ajili ya kufanyiwa matibabu zaidi.

Dokta huyo alisema baada ya kumpokea mgonjwa huyo sehemu zake za siri alizozikata hazikuwepo kabisa hata ushahidi wa kusema zilibebwa pembeni haupo.

Alisema baada ya kuziondoa aliziacha huko huko alikozikata ambapo eneo alilojikata ilibakia sehemu ya juu ya ngozi ambayo waliweza kuishona na kurudishia kawaida lakini sehemu zake za siri hazipo kabisa.

Alisema baada ya kumfanyia matibabu walichojitahidi ni kuhakikisha kwamba damu haitoki tena ikiwa ni pamoja na kushona majeraha yote pamoja na kuangalia namna ya kumpasua ili apate uwazi wa kutolea mkojo.

Aliishauri jamii kuwa makini na ndugu zao endepo watakapogundua wana matatizo ya akili au anafanya vitu ambavyo havieleweki wawapeleke kwa madaktari wanaohusika na matatizo ya akili ili kuwanusuru maisha yao.

Leah Msangi ambaye ni msimamizi wa wodi ya wanaume ambayo amelazwa kijana huyo alisema hivi sasa kijana huyo anaendelea vizuri kutokana na matibabu aliyopatiwa huku akiwashauri vijana kuwa makini na kuepuka kujiingiza katika makundi yasiyofaa ikiwemo ya uvutaji bangi.

Hata hivyo kijana huyo hakuweza kuzungumza na mwandishi wa gazeti hili kutokana na hali yake.

No comments:

Post a Comment