MAELEZO YA AWALI
Baada ya kumaliza kumi la
kwanza ambalo ni kumi la rehema, sasa tuko katika kumi la kati ambalo ni kundi
la MAGHAFIRA. Waumini wengi wameendelea kushindana na kupupia katika kufanya
ibada. Pamoja na hayo, wapo waumini waliojisahau katika kufanya ibada na hasa
Swala ya TARAWEHE
CHANZO CHA TARAWEHE
Swala ya Tarawehe ni Sunna
maarufu, inayoswaliwa baada ya Swala ya Isha, kila siku, usiku, katika Mfungo
wa Ramadhani. Na imeitwa Tarawehe, kwa sababu baada ya kila rakaa nne, watu
hupumzika, kidogo, kisha kuendelea. Na ni Swala inayo swaliwa rakaa mbili
mbili, kwa kupumzika kidogo, na baada ya kukamilisha rakaaa nne, basi
hupumzika kwa muda zaidi.
Ni Swala ambayo, siyo tu,
ameiswali Mtume mwenyewe msikitini, bali ameiswalisha jamaa, kwa muda wa siku
tatu mfululizo. Na watu walikuwa wakiongezeka kuja kuswali nyuma yake, kiasi
kwamba siku ya nne, msikiti haukutosha! Mtume hakutoka tena kwenda kuswali
Swala hiyo, licha ya watu kunadi kuwa wakati wa Swala hiyo umewadia. Mtume
hakuitikia wito wao huo. Na hakuenda msikitini, hadi alfajiri kwa ajili ya
Swala ya Alfajiri.
Aliwaswalisha Alfajiri, kama
kawaida. Lakini, alipomaliza, tu, aliwageukia waumini na kuwaeleza kwanini
hakuenda msikitini; alichelea kwamba lau angeliendelea hivyo hivyo, na watu
wakawa wanaongezeka kila siku, basi ingeliwezekana ً ikafaradhishwa Swala hiyo, juu
yao. Na wasingeliweza kutimiza jukumu hilo zito. Hivyo, akaonelea bora aswali
nyumbani, na hivyo Swala ya Tarawehe isalie kuwa ni Sunna kubwa sana, katika
Mfungo wa Ramadhani. Na alikuwa akiwahimiza sana watu kuiswali pasi na
kuwalazimisha.
Imepokewa kutoka kwa Bi. Aisha akisema: “Alitoka, Mtume
usiku mmoja akaenda kuswali msikitini. Watu wakamfuata nyuma katika Swala
yake hiyo. Kulipokucha, watu wakawa wanaambizana kuhusu swala hiyo.
Hivyo, watu wengi zaidi wakajumuika, siku ya pili.
Mtume akaenda tena usiku wa pili msikitini. Watu wengi
zaidi wakamfuata katika swala yake hiyo. Kulipokucha, watu wakaanza
kuambizana kuhusu swala hiyo. Hivyo, watu wakajumuika kwa wingi zaidi
msikitini.
Mtume akaenda tena usiku wa siku ya tatu, ambako kulikuwa na
watu wengi zaidi. Akaswali siku ya tatu, na watu wakamfuata kwa swala yake
hiyo.
Ulipoingia usiku wa siku ya nne, msikiti haukuweza kuwa na
nafasi ya kutosha watu wote waliokwenda. Mtume hakuenda msikitini. Watu
wakaanza kuita kwa kusema: “Swalaaa! Swalaaa!” Lakini Mtume hajaenda!
Ilipoingia Alfajiri ndiyo akaenda msikitini kwa Swala ya
Alfajiri.
Alipomaliza kuswali Alfajiri, aliwageukia watu na kutoa
Shahada, na kisha kusema: " Si kama nilikuwa sijui kuhusu kujumuika
kwenu jana usiku, msikitini! Nilikuwa najua vilivyo! Ila nilichelea
isije Swala hiyo ikafaradhishwa juu yenu, na halafu mkashindwa
kuitekeleza" (Bukhari na Muslim).
Inasemekana Swala hiyo ilikuwa katika Mwezi Mtukufu wa
Ramadhani.” Imepokewa kutoka kwa Abu Hurayra akisema: Amesema
Mtume “Atayefanya Ibada usiku wa mwezi (mzima) wa Ramadhani, kwa Imani
safi kabisa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu huku akiwa na matarajio ya malipo ya
Mwenyezi Mungu Pekee, atafutiwa madhambi yake yote yaliyotangulia” Muttafaq
‘alayhi. Pia Imepokewa, kutoka kwa Abu Hurayra akisema: “Alikuwa Mtume
akiwahimiza sana watu kufanya ibada usiku wa mwezi wa Ramadhani (mzima) pasi
na kuwalazimisha, kwa kusema: “Atayefanya ibada usiku wa mwezi (mzima) wa
Ramadhani, kwa Imani safi kabisa kwa Mwenyezi Mungu, huku akiwa na matarajio
ya malipo ya Mwenyezi Mungu, Pekee, atafutiwa madhambi yake yote
yaliyotangulia” (Muslim)
UMUHIMU WA SWALA HII
Kutokana na maelezo hayo hapo
juu, Swala ya Tarawehe ni Sunna kubwa sana, na ina fadhila kubwa
sana, na Mtume ameiswali, na kuswalisha msikitini. Na baada ya kuacha kwenda
kuiswalisha msikitini, watu waliendelea kuiswali katika jamaa ndogo ndogo, au
kila mtu peke yake.
Imam Bukhari amepokea Hadithi kutoka kwa Ibn Shihab, kuhusu
watu kuendelea kuswali Tarawehe, katika jamaa ndogo ndogo, au mtu binafsi,
akisema:
“Na mtindo huo ukaendela baada ya kifo cha Mtume na enzi ya
Abu Bakr na kipindi cha mwanzo cha enzi ya Umar bin al-Khattab Lakini, Umar
akaona ni vyema kuwakusanya watu wote, nyuma ya Imamu mmoja. Hivyo, akamtaka
Ubayy bin Ka’b aswalishe jamaa moja.
Imepokewa kutoka kwa Abdurrahman bin Abdulqaari’ akisema:
“Nilifuatana usiku mmoja wa Ramadhani, na Umar bin al-Khattwab kwenda
msikitini. Akaona watu wanaswali, kwa mitindo tofauti tofauti; ama wanaswali
kila mmoja peke yake, au wengine wanamfuata imamu mmoja, na wengine wanamfuata
imamu mwengine. Basi akasema: “Ya leti watu hawa wangekusanyika nyuma ya mtu
mmoja. Ingelikuwa bora zaidi!” Hivyo, baada ya hapo akaazimia kuwakusanya
waswali nyuma ya Ubayy bin Ka’b (Bukhari)
MAMBO YA KUZINGATIA
Ili Muislami apate faida
katika ibada hii ambayo pia hupatikana ndani ya mwezi huu, na kwa utukufu wa
mwezi huu hapaswi kupuuza pia azingatie kuwa:-
• Swala ya Tarawehe, au Swalat al-Layl, katika
Ramadhani, ni Sunna Muakkadah –iliyotiliwa nguvu.
• Mtume ameswali na kuswalisha Tarawehe, msikitini, kwa
muda wa siku tatu mfululizo. Na kuiswali, peke yake nyumbani.
• Mtume amehimiza Waislamu –pasi na kuwalazimisha-
kuswali Tarawehe!
• Swala ya Tarawehe inaweza kuswaliwa bila ya jamaa, au
jamaa zaidi ya moja.
• Swala ya Tarawehe inaweza kuswaliwa nyumbani au
msikitini.
• Wakati wa Swala ya Tarawehe ni baina ya kumaliza Swala
ya Isha, hadi kuchomoza alfajiri ya mwanzo.
• Kuswali Tarawehe, mara tu baada ya kumaliza Swala ya
Isha na Sunna zake, ndio bora zaidi, kwa wanaotaka kuswali jamaa.
• Kuswali jamaa moja, nyuma ya Imamu mmoja ni Sunna
kutoka kwa Mtume na vile vile, ni Sunna aliyeiendeleza, rasmi, Sayyidina Umar
nyuma ya Sayyidina Umab bin Ka’b!
• Kuswali jamaa moja, katika msikiti mmoja, nyuma ya
Imam aliyehifadhi Qur’ani, ni Sunna ilyorithiwa kutoka kwa Sayyidina
Umar
• Ubayy bin Ka’b alikuwa haafidh wa Qur’ani, na msomaji
mzuri zaidi, kwa sauti, naghama na kanuni, kuliko maswahaba wengine wote.
Mtume amesema: “Ubayy ndiye msomaji mzuri zaidi miongoni mwenu!”
• Imamu bora wa kuongoza Swala ya Tarawehe ni
aliyehifadhi Qur’ani, na mwenye sauti nzuri.
• Mwenye kusimama kufanya Ibada Usiku wa Ramadhani, kwa
nia safi, na kutaraji Fadhila za Mwenyezi Mungu tu hufutiwa madhambi yake
yaliyopita.
• Mwenye kufanya Ibada Usiku wa Ramadhani, kwa
kujionesha, au kuonesha wengine kuwa yeye ni “Mwislamu” safi, hana
anachokipata kutoka kwa Mwnyezi Mungu.
No comments:
Post a Comment