Friday, May 20, 2016

ZITTO AHOFIA KUTOWEKA KWA USAFIRI WA NDEGE NCHINI


Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe,(ACT-Wazalendo),amesema kuna hati hati ya ndege kutotua nchini kwa siku tano mfululizo kutokana na uhaba wa mafuta kwani mafuta yaliyoletwa nchini yamechakachuliwa.
Mhe.Zitto ameyasema hayo leo Bungeni,Mjini Dodoma wakati akichagia katika hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini,ambapo aliitaka serikali kueleza mikakati iliyoweka ili kukabiliana na changamoto ya ndege kutotua siku tano nchini kutokana na upungufu wa mafuta .
“Suala la uagizaji mafuta nchini hufanywa na kampuni ya wakala wa uagizaji wa mafuta kwa pamoja ambayo ipo chini ya wizara ya Nishati na Madini ambayo ndio mratibu mkuu,zabuni ilitolewa kwa kampuni ya kigeni
iitwayo MT UACC IBN AL ATHEER ya nchini Dubai ambayo ilileta mafuta ambayo yaliyoonekana yamechakachuliwa hivyo kushindwa kuingizwa sokoni na hadi sasa serikali haijachukua hatua yoyote.”anasema Mhe.Zitto
Amesema mafuta ambayo yalikuwa yaende Puma Energy peke yake yana thamani ya Dola za marekani Milioni 13, hadi leo hifadhi ya mafuta ya ndege imebakia ya siku tano tu, baada ya siku tano kama
serikali itakuwa haijachukua hatua nchi itakuwa hakuna ndege itakayotua kwa sababu hawawezi kutumia mafuta ambayo yapo nchini hivi sasa.
Pia Zitto aliomba kupata maelezo ya serikali kwamba ni hatua gani wanazochukua ili kuhakikisha suala hilo linashughulikiwa ili kupata mafuta ya ndege na ziweze kutua,lakini pia nchi isipate aibu na watalii wasishindwe kuja nchini.
Anaendelea kuhoji ni hatua gani zitachulikuliwa dhidi ya watu ambao walitoa zabuni kwenye mafuta ambayo yameonekana kuwa hayafai kutumika nchini.
“Nina barua zinazohusiana na jambo hili hivyo kama waziri atazihitaji naweza kumpatia kwa ajili ya kufanya ufuatiliaji wa suala hili na kuweza kuleta suluhisho,"anaongeza.
Kwa upande wa makampuni ya kuzalisha umeme,Zitto amesema kuna miradi ambayo imehorodheshwa na inayopaswa kuungwa mkono ambapo amesema juhudi za kwenda kwenye uzalishaji na ukuaji wa viwanda usipoendana na uzalishaji wa umeme wa kutosha zinakuwa hazina maana yoyote kutokana na kuwa kila mwekezaji anapokuja lazima aulize kama umeme upo ndipo awekeze.
Hata hivyo Waziri wa Nishati na Madini,Profesa Sospeter Muhongo,alipotafutwa ili kutoa ufafanuzi kuhusiana na jambo hilo alidai kwamba hawezi kukurupuka kulizungumizia suala hilo hadi afanye uchunguzi.

No comments:

Post a Comment