Na Lorietha Laurence-Maelezo
Baada ya kuanza rasmi kwa mabasi ya mwendo wa haraka Jijini Dar es Salaam wananchi wameupokea kwa maoni tofauti huku wengi wao wakisifia hatua hiyo ya serikali katika kurahisisha hali ya usafiri katika jiji hilo.
Wakitoa maoni yao katika maeneo mbalimbali ya jiji ,Bw.Kulwa Khamis Mfanyabiashara, mkazi wa Mbezi mwisho amesema kuwa huduma hii ya usafiri ni nzuri kwa kuwa haina foleni na inaokoa muda wa kusafiri.
“nimefurahishwa na huduma hii kwa kuwa haina foleni na inasaidia kufika kwa wakati maeneo yetu ya kazi na hata kurudi nyumbani mapema,jambo ambalo linapunguza muda mwingi uliokuwa ukipotea katika foleni” alisema Bw.Khamis.
Naye Bi.Emmy Jonas mkazi wa Kibamba amesema kuwa huduma hiyo ni nzuri lakini amedai kuwa nauli ni kubwa na kuomba uongozi wa Dar es Salaam Rapid Transport (DART) na taasisi husika kufikiria upya nauli ili wananchi wa hali ya chini waweze kumudu.
Aidha Bi. Jonas ameiomba serikali kumalizia miundombinu ya barabara ya mabasi yaendayo kwa haraka (BRT) ili yaweze kufika mpaka Kibaha, badala ya Kimara mwisho ili kuepukana na usumbufu wa kupanda magari.
Kwa upande wake Mtaalam wa Mawasiliano wa BRT, Bw. Abraham Nyatori ameiomba jamii ibadilike kuhusu utunzaji wa miundombinu,“hakuna kitu kinaitwa mali ya umma”,amesisitiza Nyatori.
Mtaalam huyo alikuwa na maana kwamba kila mwananchi anatakiwa kulinda na kuitunza miundombinu ili itumike kwa muda mrefu na kuiona kama mali yake na siyo ya umma.
Serikali imekuwa ikijenga barabara katika maeneo mbalimbali jijini na baadhi ya barabara hizo kuharibika baada ya muda mfupi na hivyo kuigharimu serikali mamilioni ya fedha kwa ajili ya matengenezo badala ya kujenga barabara zingine .
Mwisho
No comments:
Post a Comment