Na Daud Magesa, Mwanza
MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMTRA) Mkoa wa Mwanza imewafikisha mahakamani wamiliki wa vyombo vya usafirishaji wa abiria kutokana na makosa mbalimbali katika kipindi cha Machi hadi Mei mwaka huu.
Afisa Mfawidhi wa SUMATRA Michael Rodgers aliliambia gazeti hili jana katika mahojiano yaliyofanyika ofisini kwake na kueleza katika kipindi hicho mamlaka hiyo iliwakamata wamiliki 13 wa vyombo hivyo vya usafirishaji na kuwafikisha mahakamani kutokana na makosa ya ukiukwaji wa sheria za usafishaji kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa na Sumatra.
Rodgers alieleza kuwa kati ya kesi hizo tatu zilitolewa uamuzi na mahakama ikawaamuru wamiliki wa vyombo hivyo kulipa tozo (faini) ya shilingi 300,000 kila mmoja baada ya kutiwa hatiani na zingine zinaendelea kusikilizwa.
“ Tuliwakamata baadhi ya wamiliki wa magari ya biashara ya kusafirisha abiria baada ya kukiuka sheria kwa kukatisha njia kama inavyoonesha kwenye leseni zao lakini pia kwa makosa ya kufanya biashara hiyo bila ya kuwa na leseni kinyume cha sheria kifungu cha 4(3).Kati ya kesi hizo 13, tatu zilihukumiwa na wamiliki walitozwa faini ya shilingi 900,000,” alisema Rodgers.
Afisa mfawidhi huyo aliwataka wamiliki wa magari na madereva wao kuhakikisha wanazingatia sheria na kutoa huduma bora kwa wateja wao ili kuepuka usumbufu kwa pande zote mbili na kuwataka abiria kutoa taarifa pindi wanapoona hawatendewi haki na watoa huduma.
Aidha, alionya utozaji wa nauli zisizozingatia umbali kama ilivyooanishwa kwenye jedwali la nauli za magari yote ya abiria ya kwenda mikoani ama yanayotoa huduma katikati ya Jiji na wilayani, kwani wamebaini wahudumu wa magari ya daladala na yanayo kwenda wilayani wanawatoza wananchi nauli zilizo nje ya utaratibu kwa mujibu wa kigungu cha 34 cha sheria za Mamlaka hiyo.
Aliongeza kuwa wenye tabia hiyo waache kuwaumiza wananchi kwa nia ya kujipatia maslahi na faida kubwa kwa sababu nauli zilipangwa kwa kuzingatia matakwa halisiya pande zote kati ya watoa huduma na walaji, hivyo kutoza nauli nje ya utaratibu huo ni kukiuka sheria na watakaokaidi watawajibika kisheria .
No comments:
Post a Comment