Na Jovin Mihambi,Mwanza
MKUU wa Mkoa wa Mwanza Bw John Mongella (Pichani Kulia) amewataka
wafanyabiashara mkoani humo kuwekeza katika sekta ya elimu ambayo bado ina
uhitaji mwingi na shule hizo zielekezwe katika mchepuo wa masomo ya sayansi ili
serikali iweze kupata wataalamu wengi kuliko kutegemea wale kutoka nje.
Aliyasema hayo juzi (Jumapili) katika hotuba yake kwa
wahitimu wa kidato cha sita katika shule ya Alliance International Schools and
Sports Academy yaliyofanyika shuleni hapo, kata ya Mahina jijini hapa.
Alisema kuwa wafanyabiashara hao wakijenga shule hususani za
sekondari zenye mchepuo wa sayansi serikali itaweza kukidhi haja yake ya kupata
wataalamu wenye fani zinazoendana na masomo ya sayansi tofauti na ilivyo kwa
sasa ambapo wataalamu wengi ni kutoka nje ya nchi.
Alisema kuwa kwa upande wa wataalamu hususani upande wa
afya, serikali itaweza kuwa na wataalamu wengi kwa upande wa tiba na
itaondokana na kupeleka wagonjwa nje kwa ajili ya upasuaji na magonjwa mengine.
Bw Mongella alipongeza uongozi wa shule ya Alliance Schools
and Sports Academy kwa kuanzisha shule ya sekondari kidato cha tano na sita
katika mchepuo wa sayansi na kuongeza kuwa utaratibu huo unakidhi kiu ya
serikali ya kutaka kujenga shule za sekondari nyingi nchini zenye mchepuo wa
sayansi.
"Pia, mwanafunzi anapochukua masomo ya sayansi, anakuwa
na uhakika anapoingia chuoni na kuendeleza fani hiyo, huweza kupata kazi kwa
urahisi kuliko fani zingine ambazo wahitimu huangaika kutafuta kazi ambazo
hazipatikani kwa urahisi", alisema Mongella.
Kuhusu utumbuaji majipu ambayo yanafanywa na serikali ya
awamu ya tano, alisema kuwa hiyo ni sahihi kutokana kwamba baadhi ya watendaji
serikalini walikuwa wamejisahau na kufanya mambo ndivyo sivyo.
"Serikali ya awamu ya tano haina muda wa kupoteza kwa sababu
tuko nyuma sana hususani kutowashughulikiwa walaji rushwa na vitendo vingine
vya ufisadi na hatuna mda wa kuunda tume. Ukionekana umeboronga sehemu fulani
utatumbuliwa", alisema Mongella.
Naye Mkurugenzi wa Shule za Alliance Schools and Sports Academy
Bw James Bwire, alisema kuwa hapo mwakani, matarajio ya shule yake ni kufungua
chuo cha ualimu kuanzia ngazi ya cheti hadi stashahada ili kukidhi mahitaji ya
taifa na atatoa kipaumbele kwa wanachuo ambao watasomea masomo ya sayansi.
No comments:
Post a Comment