Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,Paul Makonda amezitaka Manispaa zote za Jijini humu kujenga machinjio za kisasa yatakayoweza kuzalisha nyama nyingi ambayo itachangia kuwepo kwa viwanda vya kusindika nyama hiyo.
Makonda ameyasema hayo leo wakati alipokuwa akifungua machinjio ya Vingunguti ambayo yalikuwa yamefungwa tangu Aprili 13, mwaka huu na kusema kwamba endapo kila Manispaa itajenga machinjio ya kisasa yataweza kusaidia kwa kiasi kikubwa ukuaji uchumi pamoja na kuongeza ajira kwa vijana."Tutakapojenga machinjio ya kisasa kila manispaa tutaweza kupanua masoko ya nyama kwa ndani na nje kutokana na uzalishaji mkubwa wa bidhaa hii," anasema Makonda.
Aidha amesema,kwa mujibu wa taarifa walizopewa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA)licha ya kuyafungulia machinjio hayo, lakini wanatakiwa kuyafanyia maboresho mambo yaliyobakia ikiwemo kufungua bucha katika machinjio hayo.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Vingunguti ambaye pia ni Naibu Meya wa Manispaa ya Ilala, Omari Kumbilamoto amesema,endapo itafunguliwa machinjio ya kisasa katika machinjio ya Vingunguti basi wafanyabiashara wataweza kupatiwa mikopo ya mashine za kisasa kutoka Benki ya DCB.
Anaongeza kwamba kwa mujibu wa taarifa alizopewa na Meneja Masoko na mauzo kutoka Benki ya DCB ni kuwa mashine hizo zina thamani ya sh.milioni 250 ambazo zina uwezo wa kukata nyama nyingi kwa muda mfupi."Kuanzishwa kwa tawi la benki katika eneo hilo kutaweza kutoa tija kwa wafanyabiashara kwa ajili ya kuweza kupatiwa mikopo ambayo itasaidia kunyanyua uwezo wa kipato".
Awali, TFDA iliyafungia machinjio hayo kwa sababu mbalimbali ikiwemo uchafu wa mazingira pamoja na uchakavu wa miundo mbinu.
No comments:
Post a Comment