Friday, May 13, 2016

KUPANDA BURE MABASI YA BRT NI KWA LENGO LA KUELIMISHA WATUMIAJI

Na. Immaculate Makilika- MAELEZO

ABIRIA wa mabasi ya mwendo wa haraka wametakiwa kupanda bure mabasi hayo hadi siku ya mwisho tarehe Jumapili Mei 15 mwaka huu kabla ya kuanza kutozwa nauli

Akizungumza katika kipindi Maalum cha “Malumbano ya Hoja” kilichorushwa jana (Mei 12, 2016) katika Kituo cha Televisheni cha ITV, Mkurugenzi wa Mfumo na Uendeshaji wa Wakala wa Usafiri wa Haraka jijini Dar es salaam (DART) Mhandisi John Shauri, Utaratibu huo umepangwa ili kuwawezesha watumiaji wa mabasi hayo kupata elimu ya uelewa kuhusu taratibu za huduma ya usafirishaji zinazotolewa na mabasi hayo.

Mhandisi Shauri aliwataka abiria wanaotumia mabasi hayo yanayofanya safari zake Kivukoni - Kimara, Kivukoni – Morocco, Kariakoo – Kimara na Kariakoo – Morocco kuitumia vyema fursa ya elimu ya uelewa itakayotolewa na wafanyakazi wa mradi huo walipo katika vituo vya mabasi.

Aliongeza mfumo wa usafirishaji wa mabasi umezingatia pia mahitaji ya watu wa makundi maalum wakiwemo walemavu, ambapo mwanzo na mwisho wa vituo hivyo kuna mageti maalum sambamba kutenga viti maalum ndani ya mabasi hayo vitavyotumiwa na watu wenye ulemavu.

Kwa upande wake Kamanda Mkuu wa kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Kinondoni SSP Awadhi alisema pamoja na kuwepo mradi huo sheria za barabani zinapaswa kufuatwa na waendeshaji wa mradi huo pamoja na wananchi kwa ujumla, vilevile ili wote kwa pamoja wakaelewa matumizi ya mabasi hayo na kufata utaratibu uliowekwa.

Naye Meneja Uhusiano wa UDA, Bwana Dennis Mgaya aliwataka abiria wapande mabasi hayo kwa kutumia vituo vilivyopo kwa dhamira ya kujifunza, badala ya kutumia muda mwingi kuzunguka ndani ya mabasi hayo.



Jumla ya mabasi yaendayo haraka 138 yamewasilia nchini kwa ajili kutoa huduma ya usafirishaji kwa jiji la Dar es salaam ili kupunguza msongamano kwa wakazi wa jiji hilo, na tayari mabasi hayo yameanza kutoa huduma tangu mwanzo wiki.

No comments:

Post a Comment