Tuesday, April 12, 2016

TRICKSTER YALETA SHINDANO LA BIASHARA NCHINI, YASHIRIKISHA NCHI 5

Na Maelezo

Kampuni ya Kijapani inayofanya shughuli zake nchini (Trickster) imeandaa shindano la wazo la biashara litakalozishirikisha nchi tano za Afrika zikiwemo Kenya,Rwanda,Zambia,Zimbabwe na Tanzania mwenyeji wa mashindano hayo kwa mwaka 2016.

Akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Meneja Mradi kutoka kampuni ya Afrika New Business Development Department(DMM) Bw.Alex Kapungu ambao ndio wadhamini wa shindano hilo ameeleza kuwa lengo la shindano hilo ni kusaidia kuboresha ujasiriamali katika bara la Afrika.

“Shindano hili linafanyika kwa mara ya kwanza na hivyo ni fursa nzuri kwa wajasiriamali na wale wanaotaka kuwa wajasiriamali kushiriki na baadaye kufanikisha wazo hilo kiutendaji kwa kuwa biashara halisi”alisema Bw.Alex.

Aidha ameongeza kuwa vigezo vya kushiriki shindano hilo ni mshiriki awe amefikisha miaka 18 na kuendelea, awe anajua kuongea na kuandika lugha ya kiingereza na kuwa na hati ya kusafiria.

Naye Mkurugenzi wa Trickster Bw.Sonobe Atsushi amesema washindi watakaoingia nusu fainali watapata fursa ya kutembelea nchi ya japani ambapo mshindi wa kwanza atapata fedha taslimu Dola elfu tano za kimarekani.

Pia ametoa wito kwa watanzania kujitokeza na kushiriki kwa wingi ili wapate fursa ya kuanzisha biashara kupitia mawazo watakayoyatoa na hivyo kupanua wigo wa biashara.




No comments:

Post a Comment