Monday, April 11, 2016

AFRIKA: BEI ZA CHINI ZA BIDHAA ZINAENDELEA KUKWAMISHA UKUAJI UCHUMI


WASHINGTON, Aprili 11, 2016 — Shughuli za kiuchumi katika bara la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara zilidorora katika mwaka 2015, wakati ukuaji wa Pato Ghafi la Taifa ukiwa wa wastani wa asilimia  3.0, ikishuka kutoka asilimia 4.5 mwaka 2014. Hii ina maana kwamba kasi ya ukuaji uchumi imepungua hadi kufikia viwango vya chini tulivyovishuhudia kwa mara ya mwisho mwaka 2009.
 
Takwimu hizi zimewasilishwa kwa muhtasari katika ripoti ya Africa’s Pulse (Mapigo ya Damu ya Afrika), huu ni uchambuzi wa kila nusu mwaka unaofanywa na Benki ya Dunia wa mienendo ya kiuchumi na takwimu za hivi karibuni kwa bara hili. Makisio ya ukuaji kwa mwaka 2016 yanabaki kuwa chini katika asilimia 3.3, kiwango ambacho kiko chini sana ukilinganisha na ukuaji imara wa Pato Ghafi la Taifa kwa asilimia 6.8 ambao bara liliuendeleza kwa kipindi cha 2003-2008. Kwa ujumla, ukuaji wa uchumi unatarajiwa kuongezeka katika mwaka 2017-2018 kufikia asilimia 4.5.
 
Kushuka kwa bei za bidhaa – hususani mafuta, ambayo yalishuka kwa asilimia 67 kutoka Juni 2014 hadi Desemba 2015 – na mdororo wa uchumi duniani, hasa katika chumi za masoko yanayoibukia, ndio sababu za bara kufanya vibaya kiuchumi. Mara nyingi, athari hasi za bei za chini za bidhaa zimeongezewa nguvu na mazingira mabovu ya ndani ya nchi kama vile mgawo wa umeme, sera zisizo na uhakika, ukame, na vitisho vya usalama, ambavyo vyote vimekwaza ukuaji uchumi. Kuna baadhi ya maeneo ambako uchumi umeendelea kukua kwa nguvu kama vile nchi ya Ivory Coast, ambayo inajivunia mazingira mazuri ya sera na kuongezeka kwa uwekezaji, pia na nchi zinazoagiza mafuta kama vile Kenya, Rwanda, na Tanzania.

 
Mazingira ya nje yanayolikabili bara yanatarajiwa kuendelea kuwa magumu. Katika nchi nyingi, ulinzi wa kisera ni dhaifu, hivyo kupunguza mwitikio wa sera wa nchi hizi. Ucheleweshaji wa kutekeleza marekebisho ya kuanguka kwa mapato kutokana na mauzo ya bidhaa nje ya nchi, na hali ya ukame inayozidi kuwa mbaya ni vitu vinavyohatarisha matarajio ya ukuaji wa uchumi kwa bara la Afrika.
 
”Wakati nchi zinajirekebisha kukabiliana na mazingira ya dunia yenye changamoto nyingi, juhudi madhubuti zitahitajika kuongeza uhamasishaji wa rasilimali za ndani. Wakati mwenendo wa kushuka kwa bei za bidhaa ukiendelea, hususani mafuta na gesi, huu ni muda muafaka kwa kuzidisha kasi ya mageuzi yote ambayo yatazibua uwezo wa kukua kwa uchumi wa Afrika na kuwapatia watu wa Afrika umeme nafuu,” anasema Makhtar Diop, Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia kwa Afrika.
 
Nchi nyingi zinatarajiwa kuwa na ukuaji wa uchumi wa wastani. Miongoni mwa masoko mapya, ukuaji uchumi unatarajiwa kuongezeka nchini Ghana, unaosukumwa na kuboreshwa kwa hisia chanya za wawekezaji, kuzinduliwa kwa visima vipya vya mafuta, na kupungua kwa matatizo ya umeme. Nchini Kenya, ukuaji uchumi unatarajiwa kuendelea kuwa imara, ukichangiwa na matumizi katika sekta binafsi na uwekezaji wa umma kwenye miundombinu.
 
Ongezeko la shughuli linalokisiwa katika mwaka 2017-2018 linaakisi maboresho ya taratibu katika chumi kubwa zaidi katika bara – Angola, Nigeria, na Afrika Kusini – wakati bei za bidhaa zikitengemaa na maboresho ya kukuza uchumi yakitekelezwa.
 
 
Majiji ya Afrika kama Injini za Kukuza Uchumi
 
Wakati Afrika inapita katika kipindi cha ukuaji wa kasi wa miji yake, kuna dirisha la fursa la kutumia uwezo wa majiji haya kama injini za ukuaji. Kushuka kwa haraka kwa bei za bidhaa na mafuta kumekuwa na athari hasi kwa nchi zinazozalisha bidhaa hizo na hivyo kuashiria haja ya haraka ya kujenga uchumi anuwai katika bara la Afrika. Kukua kwa miji inayosimamiwa vyema kunatoa fursa kubwa ya kuwa kichochezi cha uchumi anuwai.
 
Ukuaji wa majiji, kama utasimamiwa vyema, unaweza kusukuma ukuaji wa uchumi na tija. Lakini majiji ya Afrika kwa sasa hayajengi chumi za mkusanyiko au kuvuna faida za tija za mijini. Badala yake yanasumbuliwa na gharama za juu za makazi na usafiri, aidha na gharama za juu za chakula ambazo zinatumia sehemu kubwa ya bajeti za kaya za mijini.
 
Makazi na usafiri ni yenye gharama kubwa hususani katika miji ya Afrika. Bei za makazi ni takribani asilimia 55 juu zaidi katika maeneo ya mijini ya nchi za Kiafrika ukilinganisha na viwango vyao vya kipato. Usafiri mijini, ambao unajumuisha bei ya magari na huduma ya usafiri, ni takribani asilimia 42 ghali zaidi katika miji ya Afrika kuliko ilivyo katika nchi nyingine. Kama ilivyo kwa kaya na wafanyakazi, makampuni pia hukabiliwa na gharama za juu za mijini. Uchambuzi wa nchi kwa nchi unathibitisha kwamba viwanda vinavyozalisha katika majiji ya Afrika hulipa mishahara ya juu zaidi kwa vigezo vya thamani halisi ya pesa kuliko makampuni katika miji ya nchi nyingine ambazo ziko katika viwango sawa vya maendeleo.
 
Ili kujenga miji ambayo inafanya kazi—miji ambayo watu huweza kuishi, inayofikika, yenye unafuu wa maisha, na hivyo kuwa na uchumi imara—watunga sera watahitaji kuelekeza nguvu zao katika matatizo ya ndani zaidi ya kimfumo, ambayo hayatengi ardhi, yanavuruga maendeleo, na kukwaza tija.
 
Ili kuhakikisha ukuaji uchumi na maendeleo ya kijamii, miji inahitaji isiwe ya gharama kubwa kwa makampuni na iweze kuwavutia zaidi wawekezaji,” anasema Punam Chuhan-Pole, Kaimu Mchumi Mkuu, Benki ya Dunia katika Afrika na mtunzi wa ripoti hii. “Pia ni lazima iwe inawajali wakazi, kuwapatia huduma, mahitaji. Yote haya yatahitaji kufanya maboresho ya masoko ya ardhi ya mijini na kanuni za miji na kuratibu uwekezaji wa miundombinu katika hatua za awali.”
 
Vigezo vya biashara
 
Kushuka kwa bei za bidhaa kumeshusha vigezo vya biashara vya Afrika kwa mwaka 2016 kwa takribani asilimia 16, wakati wasafirishaji wa bidhaa nje wakipata hasara kubwa kwa bidhaa zao. Katika bara zima kwa mwaka 2016, athari za mtikisiko huu unatarajiwa kushusha ukuaji wa uchumi kwa asilimia 0.5 kutoka kwenye msingi, na kudhoofisha mapato halisi na urari wa fedha kwa takribani asilimia 4 na 2 juu ya msingi.
 
Kusonga Mbele
 

Nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara zitaendelea kukabiliwa na bei za chini na zinazobadilika badilika katika masoko ya bidhaa duniani. Serikali lazima zichukue hatua za kujirekebisha kuja kwenye bei mpya za chini za bidhaa, kushughulikia udhaifu wa kiuchumi, na kujenga vyanzo vipya vya ukuaji uchumi ulio endelevu na jumuishi. Miji ya Afrika inayokua inatoa chachu ya kujenga uchumi anuwai. Lakini inahitaji taasisi bora za kupanga mipango athirifu na uratibu ambao utaweza kuinua wingi wa shughuli za kiuchumi mijini na tija, na hivyo kuchochea mageuzi ya bara.


No comments:

Post a Comment