Tuesday, April 05, 2016

FASTJET YASITISHA SAFARI KILIMANJARO-NAIROBI






Dar es Salaam, Aprili 4, 2016 -Fastjet Tanzania imesitisha safari zake kati ya Kilimanjaro na Nairobi.

Fastjet ilikuwa ikifanya safari kutoka Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro kwenda Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta Nairobi mara mbili kwa wiki siku za Ijumaa na Jumapaili.

Kusitishwa kwa safari kwenye njia hiyo kunatokana na kuwepo mahitaji haba ya abiria kwenye masoko yote mawili ya Kilimanjaro na Nairobi hali iliyosababisha kutokuwa na manufaa kibiashara.

Shirika hilo limeeleza kuwa lengo lake ni kuhakikisha linarudisha safari hizo kati ya Kilimanjaro- Nairobi pindi tu na wakati ambapo wateja wataihitaji. Safari za fastjet kutoka Dar es salaam na Kilimanjaro kwenda Nairobi zilianza Januari 11, 2016.



Mahitaji ya abiria kwa safari hizo ambazo kwa kiwango kikubwa ni za kibiashara kati ya majiji ya Dar es Salaam na Nairobi ambayo kwa pamoja yana idadi ya watu ambao ni zaidi ya milioni nane yamekuwa makubwa na kuifanya fastjet hivi karibuni kuongeza safari zake kwenye njia hiyo ili kukidhi mahitaji makubwa ya abiria.

Fastjet kwa hivi sasa inafanya safari mbili za kwenda na kurudi kati ya miji hiyo kila siku ndani ya wiki na hivyo kufanya jumla ya safari zake kwa wiki kati ya Uwanja wa Kimataifa wa Dar es Salaam na Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta kuwa ni 28.

Mtiririko mpya wa safari unawapatia wateja huduma sahihi mapema nyakati za asubuhi na jioni na matokeo ya ratiba hiyo ni kuwepo kwa takribani viti 19,000 kila mwezi kwenye safari hizo kati ya majiji hayo mawili na hali kadhalika kuwapatia wateja mbadala sahihi wa kusafiri kwa nauli wanayoimudu.

Nauli za fastjet kimsingi ni za chini ikilinganishwa na tozo za mashirika mengine ambayo kwa sasa yanafanya safari zake kati ya Kenya na Tanzania.

Nauli kutoka Tanzania kwenda Kenya zinaanzia shilingi 176,000 kwa safari moja, bila kodi ambayo ni shilingi 107,800 kwa kuondokea Tanzania na dola 40 kwa kuondokea Kenya, na hivyo fastjet kuwashauri abiria kukata tiketi zao mapema kabla ya siku ya kuanza safari ili kutumia fursa hiyo ili kufaidi na nauli ya chini.

Nauli kutoka Kenya zinaanzia dola za Marekani 120 kwa safari moja zikijumuishwa kodi za serikali ambayo ni dola 40 kwa kuondokea Kenya.

Matokeo ya safari hizi kati ya Nairobi na Dar es Salaam yamekuwa ni makubwa kutokana na ukweli unaojidhihirisha kwamba nauli kwenye mashirika shindani yanayofanya safari kati ya nchi hizi mbili zimeshuka kwa kiwango cha asilimia 40 tangu fastjet ianzishe safari zake.

Fastjet inasisitiza kwamba kupunguza mtiririko wa safari kwenye njia kati ya Nairobi na Kilimanjaro kunafungua fursa ya kuongeza uwezo zaidi kwa njia zilizopo kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na hali kadhalika kuwepo uwezekano wa kufungua njia nyingine mpya siku za karibuni.

No comments:

Post a Comment