Na MAELEZO
Dar es Salaam.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imetoa tamko kuhusu hali ya
wakimbizi nchini kuanzia mwezi Aprili mwaka 2015 hadi tarehe 10 Februali, 2016.
Akitoa tamko hilo leo jijini Dar es salaam Msemaji wa Wizara
hiyo Isaac Nantanga amesema kuwa Serikali imekuwa ikipokea raia
toka Burundi wanaoingia nchini Tanzania kutokana na machafuko yaliyotokea
nchini humo.
“Kiasi cha wakimbizi 129,210 toka nchini Burundi wameingia
nchini kuomba hifadhi kutokana na machafuko yaliyotokea nchini mwao
tangu mwezi Aprili mwaka jana hadi sasa” alisema Nantanga.
Nantanga ameongeza kuwa kati ya wakimbizi 129,210, wakimbizi
79,290 wanahifadhiwa katika kambi ya wakimbizi Nyarugusu Mkoani Kigoma na
wengine 45,487 wanahifadhiwa katika kambi ya wakimbizi ya Nduta iliyopo
Wilayani Kibondo na 4,543 wanahifadhiwa katika kambi ya wakimbizi Mtendeli
iliyopo Wilayani Kakonko.
Ameeleza kuwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa
kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) na
wadau wengine imekuwa ikitoa huduma muhimu kama vile za afya, chakula, maji na
ulinzi ili kuhakikisha wakimbizi wanaishi kwa usalama.
Mbali na hayo Tanzania inawakimbizi wengine ambao wapo
katika kambi ya Nyarugusu ikijumuisha Wakongo 61,887, Wasomali 150 na wengine
189 toka katika nchi mbalimbali na kupelekea nchi ya Tanzania kuwa na jumla ya
wakimbizi 191,436 ambao wamehifadhiwa katika makambi.
Wizara ya Mambo ya Ndani imeendelea kushughulikia Raia wa
nchi za nje walioomba vibali cha kupatiwa hifadhi ya ukimbizi, hivyo maombi 815
yameshashughulikiwa na Kamati ya Kitaifa kuona kama wanastahili kupewa hadhi ya
ukimbizi.
No comments:
Post a Comment