Na MAELEZO.
Naibu Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Anastazia Wambura amezitaka jamii kutoa elimu ya jando na unyago kwa kuzingatia umri na wakati sahihi wa mafunzo hayo ili kuweza kuondoa tatizo la mimba na ndoa za utotoni.
Ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati alipozungumza na Wawakilishi wa asasi za kiraia kutoka mkoani Mtwara wanaoshughulika na mapambano dhidi ya mimba na ndoa za utotoni zinazosababishwa na utekelezaji wa wa mila na desturi hizo mkoani Mtwara.
“Ni vizuri kuwafundisha watoto wetu maadili mema wakiwa wadogo,lakini ni vizuri Kuandaa namna ya kutoa elimu kwa kuzingatia umri na aina ya elimu ili kutoa taaluma hiyo kwa watu sahihi na wakati unaofaa. Alisema Mhe.Anastazia.”
Mwenyekiti wa asasi hizo Dkt.Lillac Malumbo akitoa taarifa ya jinsi wanavyoshughulikia tatizo hilo amesema kuwa asasi zinatoa mafunzo mbalimbali kwa kwa wakufunzi wa watoto wa kike ili kupunguza tatizo la mimba za utotoni linalosababishwa na utekelezaji wa mila mbalimbali mkoani Mtwara.
“Tunaamini kuwa jamii ikielimishwa kuhusu madhara yatokanayo na baadhi ya mada zinazotolewa katika mafunzo ya unyago na ambazo zinaleta ushawishi kwa watoto wa kike kujiingiza katika zinaa, mimba na ndoa za utotoni tatizo ili litaisha.Alisema Dkt. Lillac.”
Dkt Lillac ameongeza kuwa kuweka ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na asasi hizo kutamuwezesha mtoto wa kike kupata elimu, kuepuka magonjwa ya Zinaa ,kupunguza watoto yatima na watoto wa mtaani.
Hata hivyo mila hizi zimekuwa zikiwanyima watoto wa kike haki ya kupata elimu kwa wakati, kusikilizwa, kuendelezwa na kuwafanya kubaki tegemezi kwa muda wote.
Asasi hizi zinatoka katika wilaya nne za mkoa wa Mtwara ambazo ni Tawaso Masasi,Msoapo Mtwara,Aware Mtwara vijijini ,Chakumuma Masasi,Nyerere Tandahimba,Kimweso Mtwara vijijini, pamoja na Children Youth Development Innitiatives (CYDI).
No comments:
Post a Comment