Friday, February 26, 2016

WAZIRI NAPE AAHIDI UPATIKANAJI WA SERA YA FILAMU NCHINI.

Na Maelezo.
Katika kuhakikisha kuwa Sekta ya Filamu nchini inakua kwa kasi na kuleta manufaa kwa wasanii, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye amewahakikishia wasanii juu ya kupatikana kwa Sera ya filamu ili kuleta matokeo chanya ya katika kazi zao.

Mhe. Nnauye ameyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa uchaguzi wa viongozi wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) ambapo ameahidi kushirikiana na Shirikisho hilo katika nyanja mbalimbali na kuwataka wanachama kuchagua viongozi wawajibikaji watakaoweza kusimamia Katiba kwa maslahi ya wote.

“Chagueni viongozi wenye weledi, wawajibikaji na wachapakazi ili mshirikiane nao katika kuleta maendeleo kutokana na kazi zenu kitaifa na kimataifa”, alisema Mhe. Nnauye.

Aidha, Mhe. Nnauye ameahidi kutatua tatizo la usambazaji wa kazi feki za filamu ulioenea kwa kasi nchini ambapo amesema kwa kushirikiana na wadau wa filamu nchini yaani Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bodi ya Filamu pamoja na COSOTA watahakikisha kuwa, kazi ambayo haina ubora haingii sokoni.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu, Bi. Joyce Fissoo ameeleza kuwa, Serikali itasimamia kwa umakini filamu za nchini kwa kutoa mafunzo kwa vijana na Shirikisho ili waelewe majukumu yao na jinsi ya kufanya kazi kwa weledi.

Bi. Fissoo ameongeza kuwa nidhamu katika kazi ni muhimu kwa wasanii kwa kuwa inaleta heshima kwao na kwa Taifa, hivyo ni wajibu wa kila msanii kufuata maadili ili kuzalisha kazi nzuri zitakazopata soko ndani na nje ya nchi.

“Kuwepo katika Vyama ni msingi mkubwa wa mafanikio, fuateni Katiba, tafuteni vipaumbele katika kazi zenu na pia zingatieni muda kwa kila mtakalofanya, naamini mtafanikiwa’’, alisema Bi. Fissoo.

Shirikisho la Filamu Tanzania lilifanya uchaguzi wa Rais, Makamu wa Rais na wajumbe kumi wa Bodi Februari 25 mwaka huu, ambapo Bw. Simon Mwakifwamba alitetea nafasi yake ya kiti cha Urais wa Shirikisho hilo kwa muhula wa miaka mine (2016-2020) na Bw. Deo Sanga kuwa makamu wa Rais.

No comments:

Post a Comment