Friday, February 26, 2016

BADILISHENI SERA MUANDIKE HABARI CHANYA KWA WATU WENYE ULEMAVU: DKT POSSI























Naibu waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu wenye Ulemavu) Dkt Abdallah Possi akizungumza na Wamiliki na wahariri wa vyombo vya habari leo ofisini kwake Jijini Dare s salaam.(Picha na Raymond Mushumbusi)

Na Joseph Ishengoma
Naibu waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu wenye Ulemavu) Dkt Abdallah Possi ameviagiza vyombo vya habari nchini kuwa na sera katika vyombo vyao inayojumuisha uandishi wa habari chanya kwa watu wenye ulemavu.


Akitoa agizo hilo mbele ya wamiliki wa vyombo vya habari leo Ofisini kwake Jijini Dar es Salaam Waziri Possi amesema habari nyingi zinazohusu watu wenye ulemavu ni za kuwanyanyapaa na kuonesha kuwa hawana uwezo wa kufanya mambo chanya.

“Wekeni kipengele katika sera zenu kitakachosaidia kuwaelimisha watu kuwa watu wenye ulemavu ni sehemu ya jumuiya katika maisha ya kila siku ya wanadamu,” amesema. Kwa mujibu wa Waziri Possi, vyombo vya habari vikiwa na sera iliyowazi na kuitekeleza, watu watabadilika na kupata taarifa nzuri za watu wenye ulemavu.

Dkt. Possi ameeleza kuwa taarifa za watu wenye ulemavu hazitakiwi kuwa na lugha zenye chembechembe za kunyanyapaa. Amesema kuwa kila kituo cha televisheni kinatakiwa kuwa na wataalamu wa kutafsiri habari na vipindi muhimu kwa lugha za alama.

KUSHOTO: Mhadhiri toka Chuo Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam Shule ya Uandishi wa Habari Dkt Harub Riyoba (katikati) akimsikiliza Naibu waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu wenye Ulemavu) Dkt Abdallah Possi alipokutana na Wamiliki wa Vyombo vya habri kulia ni Mkurugenzi wa Uendeshaji toka Azam Media Yahya Mohamed na kushoto ni Meneja wa Uendeshaji toka Sahara Media Steve Diallo.

Amesema, “Serikali kwa kutumia Sheria ya Watu wenye ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010 inaandaa tangazo kuvikumbusha vyombo vya habari kuwa kuwa na wataalam wa kutafsiri habari na vipindi muhimu kwa lugha za alama kwa watu wenye ulemavu.”

Aidha Naibu Waziri amewaagiza wamiliki wa vyombo vya habari kutoa ajira kwa watu wenye ulemavu kwani Sheria inaagiza lazima chombo chochote chenye wafanyakazi zaidi ya 20, angalau mfanyakazi mmoja awe mtu mwenye ulemavu. Kwa upande wao wamiliki wameiomba serikali kutotoza kodi tangazo lolote linalohusu habari chanya za watu wenye ulemavu.

Hata hivyo wamiliki hao wamemweleza Naibu Waziri kuwa ubadilishaji wa Sera pamoja na kuwa na wataalam wa kutafsiri habari na vipindi muhimu kwa watu wenye ulemavu ni jambo zuri, lakini wanahitaji kupewa muda wa maandalizi.






No comments:

Post a Comment