Kulwa Mayombi, EANA
Arusha, 8 Februari, 2016 (EANA)
Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) imeendelea kuongeza wanachama baada ya nchi ya Chad kuridhia itifaki iliyoanzisha Mahakama hiyo yenye makao yake makuu jijini Arusha.
Hatua hiyo inafanya Chad kuwa nchi ya 30 kuridhia itifaki hiyo kati ya nchi 54 wanachama wa Umoja wa Afrika (AU).
Hata hivyo, kati ya nchi hizo 30, ni nchi 7 tu ndizo zilizotoa tamko la kukubali mamlaka ya Mahakama ya Afrika kuweza kupokea kesi za watu binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) kwa mujibu wa kifungu cha 34(6).
Nchi hizo zilizotoa tamko hilo ni pamoja na wenyeji Tanzania, Burkina Faso, Ivory Coast, Ghana, Malawi, Mali na Rwanda.
Mwezi Desemba mwaka jana 2015, Rais wa Chad Idris Deby aliahidi nchi yake kuwa itaridhia itifaki alipokutana na Rais wa Mahakama hiyo Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania Augustino Ramadhani katika semina ya kuitambulisha mahakama hiyo kwa wadau mbalimbali kutoka nchi za Afrika ya kati iliyofanyika mjini N’djamena.
Mahakama ya Afrika ilianzishwa kwa mujibu wa kifungu namba moja cha itifaki ya mkataba wa mahakama hiyo ili kuimarisha jukumu la kulinda haki za tume ya Afrika ya Haki za binadamu na watu barani Afrika.
Mafanikio ya Mahakama hiyo kama chombo cha kulinda haki za binadamu yanahitaji nchi nyingi zaidi wanachama wa AU kuridhi itifaki and tamko ili kutoa mamlaka ya kushughulikia kesi zinazoletwa mbele ya Mahakama.
No comments:
Post a Comment