Monday, January 11, 2016

UNESCO YAPENDEKEZA SILAHA ZIDHIBITIWE HARAKA NYARUGUSU


Kutoka kushoto Rehema Horera wa UNESCO, Sospeter Boyo Mkuu wa Makazi ya Ulyankulu na Emmauel Mlule wa UNESCO Tume ya Taifa    

Na ImmaMatukio

Tume ya Taifa ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) imependekeza kuwa, kuna haja ya hatua za haraka kuchukuliwa ili kudhibiti kuzagaa kwa silaha ambazo huatarisha usalama wa wakimbizi pamoja na nchi kwa ujumla.

Pendekezo hilo imelitoa baada ya kufanya ziara katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu iliyopo wilayani Kasulu Mkoa wa Kigoma ili kubaini mambo mbalimbali kuhusu mahitaji na changamoto za wakimbizi hapa nchini.

Ujumbe huo wa UNESCO ulionesha umuhimu wa kudhibiti mapema ili kukomesha vitendo vya ujambazi na utekaji ambavyo ni tishio kubwa kwa amani ya wakazi na hata watendaji wa mashirika mbalimbali katika makazi hayo ya Nyarugusu.

Katika ujumbe huo, UNESCO iliwakilishwa na maofisa wa Programu ya Sayansi ya Jamii, Rehema Horera na Emmanuel Mlule ambao kwa pamoja wametoa wito kwa wadau wote kuchangia kuleta hali bora kwa jamii ya wakimbizi ambao kama binadamu wengine mahitaji na haki zao za msingi zinapaswa kutekelezwa, kulindwa na kuendelezwa.

Katika kikao cha pamoja na uongozi wa wakimbizi katika kambi ya Nyarugusu, Mwenyekiti wa Wakimbizi kambini hapo, Abilola Angelique alieleza kuwa;

“Maisha ya kambini popote ni magumu. Hatuna uhuru wa kutosha kujishughulisha na hata kupata habari, tunahitaji kuangaliwa hasa katika masuala ya elimu, afya, chakula, mavazi na hata haki za jinsia hasa kwa wanawake” .

Akitoa maelezo juu ya hali ya wakimbizi katika eneo lake,Mkuu wa Makazi ya Wakimbizi ya Nyarugusu, Sospeter Boyo alisema kuwa mahitaji na changamoto za wakimbizi zinafanana kwa kiasi kikubwa katika kambi zote na za wakimbizi waliopo Nyarugusu.

“Changamoto kubwa zinahusu elimu, maji, mahusiano na wenyeji, mahitaji ya kiafya na pia hali ya ulinzi, usalama na amani katika eneo la wakimbizi na mkoa mzima,” alisema.

Kwa upande wake Mratibu wa Wakimbizi wa Kanda ya Kigoma,Tonny Laiser alishukuru zoezi hilo na kusisitiza ushirikiano katika kukabiliana na changamoto za masuala ya wakimbizi kati ya watendaji wote na taasisi zingine kwani jitihada za Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) na mashirika mengine hazitoshi ikizingatiwa kuwa idadi na mahitaji ya wakimbizi yanaongezeka kila kukicha.

Katika hatua nyingine, Katibu wa Wakimbizi kambini hapo, Maua Ernide ambaye pia ni mwakilishi wa Umoja wa Wanawake kambini hapo alishukuru kutembelewa na wawakilishi hao wa Tume ya Taifa ya UNESCO.

“Hatujawahi kamwe kutembelewa na shirika hili tunashukuru Mungu leo (hivi karibuni) mmetufikia kwa sababu tunaifahamu UNESCO, tuna mahitaji makubwa sana ya elimu kwa watoto na hata sisi watu wazima,” alisema.

Kwa kipindi kirefu Tanzania imekuwa ikipokea idadi kubwa ya wakimbizi kutokana na machafuko ya kisiasa yanayosababisha raia wa nchi jirani kukimbia nchi zao.

Nyarugusu ni makazi ya wakimbizi kutoka nchi za Kenya, Uganda, Sudani Kusini, Somalia, Rwanda, Burundi, Ethiopia, Zimbabwe na Ivory Coast.


Kutoka kushoto ni Emmanuel Mlule wa UNESCO, Rehema Horera wa UNESCO na kulia ni Tonny Laiser Mratibu wa Idara ya Wakimbizi Kanda ya Kigoma


Rehema Horera na Emmanuel Mlule wakiwa na wawakilishi wa uongozi wa wakimbizi kambi ya wakimbizi makazi ya Nyarugusu


No comments:

Post a Comment