Na MAELEZO
Serikali imetolea ufafanuzi kuhusu taarifa za upotoshaji kwa
umma kuwa imefuta vipindi vya shughuli za Bunge kuoneshwa katika televisheni ya
Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC) kama zisemazo taarifa zilizozagaa
mitaani.
Hayo yamesemwa jana Mjini Dodoma na Waziri wa
Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Nape Mose Nnauye wakati akiongea na
wananchi moja kwa moja kupitia vyombo mbalimbali vya habari nchini kutolea
ufafanuzi taarifa za upotoshaji juu ya TBC kufuta vipindi vya matangazo ya
vikao vya Bunge.
Mhe.Nape Moses Nnauye amesema Serikali haijafuta vipindi vya
Bunge bali ilichofanya ni kubadilisha muda wa kurusha vipindi hivyo kutoka muda
wa mchana na kuviweka usiku kwa lengo la kupunguza gharama za kurusha moja kwa
moja matangazo hayo ya Bunge na pia kuwapa fursa wananchi zaidi kuangalia
na kufatilia yanayoendelea Bungeni kwa kuwa muda wa usiku watu wengi wanakuwa
wamesharejea kutoka katika shughuli zao za ujenzi wa taifa.
Ameongeza kuwa Serikali imechukua uamuzi wa busara katika
hili kwani TBC inatumia Sh Billion 4.2 kwa mwaka kama gharama za urushaji wa
moja kwa moja wa matangazo hayo , hivyo itasaidia katika kubana matumizi ya
shirika hilo kwani fedha hizo hazipo katika bajeti ipewayo shirika bali ni
fedha za ndani zinazokusanywa na shirika hilo.
Aidha amesema kuwa sio kitu kigeni kwa Bunge kutotangazwa
moja kwa moja kwani kuna baadhi ya mabunge katika nchi nyingine urekodiwa na
kurushwa baadae kama kipindi maalum cha Bunge,amezitaja baadhi ya nchi hizo
kuwa ni New Zealand, India, Malawi, Lesotho, Uingereza na Singapore.
Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC) lilianza kurusha
matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania mwaka 2005 ila baada ya Serikali kukaa na kujadili kwa kina
kuhusu gharama za urushaji wa matangazo hayo moja kwa moja ikaamua kubadili
mtindo wa urushaji wa matangazo hayo kutoka matangazo ya moja kwa moja kwa siku
nzima kwenda kwenye mfumo wa kuyarekodi na kuyarusha katika kipindi cha LEO KATIKA
BUNGE.
No comments:
Post a Comment