Wednesday, August 26, 2015

TAARIFA KUHUSU RATIBA YA KAMPENI ZA UCHAGUZI MKUU



Kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge za mwaka 2015 pamoja na Maadili ya Uchaguzi ya mwaka 2015. Kampeni za Uchaguzi huanza siku moja baada ya uteuzi na huisha siku moja kabla ya siku ya kupiga Kura.

Kwa madhumuni ya kuhakikisha kuwa Kampeni zinafuata muda, Kanuni ya 39 (2) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge pamoja na Maadili ya Uchaguzi kifungu cha 2.1 (c) inaelezwa Mikutano yote ya Kampeni itaanza saa 2:00 asubuhi n kuisha saa 12:00 jioni.

Kanuni ya 40 (1) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge za mwaka 2015 inasema, Mkurugenzi wa Uchaguzi kabla Kampeni za Uchaguzi wa Rais hazijaanza atavitaka vyama vya Siasa kuwasilisha mapendekezo ya ratiba za Mikutano ya Kampeni, na kanuni ndogo ya (3) inasema, lazima Chama kiwasilishe mapendekezo ya Ratiba ya Mikutano ya Kampeni ikionesha tarehe, muda, Mkoa na Wilaya ambapo Mkutano utafanyika.

Aidha, kanuni ya 41 (1) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge za mwaka 2015 inaeleza kuwa iwapo Chama cha Siasa kitahitaji kufanya mabadiliko ratiba au eneo la Mkutano wa Kampeni, kitawasilisha mapendekezo yakiambatishwa na sababu za kutaka kufanya mabadiliko kwa Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, ambaye kabla ya kufanya marekebisho katika Ratiba husika ataitisha Mkutano wa Kamati ya Kuratibu Ratiba ya Kampeni za Uchaguzi wa Rais inayojumuisha vyama vyote vyenye wagombea katika nafasi hiyo ili vikubali au kukataa mabadiliko yanayopendekezwa.

SOMA ZAIDI. . .

Kwa kuzingatia matakwa ya Kanuni tajwa hapo juu, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilivialika Vyama vya Siasa vyenye Wagombea wa kiti cha Rais kuwasilisha mapendekezo ya Ratiba ya Mikutano ya Kampeni ya Rais. 

Mnamo tarehe 22 Agosti, 2015 kwenye kikao cha kwanza cha Tume ya Taifa ya Taifa ya Uchaguzi, Vyama vyote vyenye Wagombea wa Kiti cha Rais vilipitia mapendekezo ya Ratiba ya Mikutano ya Kampeni ya Wagombea Kiti cha Rais ambapo marekebisho yalifanyika na kwa pamoja vyama vilikubaliana kuwa Ratiba hiyo ndiyo itakayofuatwa hadi hapo kutapotokea marekebisho yatakayokubaliwa na vyama vyote vye Wagombea wa kiti cha Rais.

Aidha, kwa mujibu wa Kifungu cha 124A (1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa madhumuni ya kuendesha Uchaguzi wa haki, uhuru na Amani, na baada ya kushauriana na Vyama vya Siasa na Serikali, itaandaa Kanuni za Maadili ya Uchaguzi yatayoeleza maadili ya vyama vya siasa na Tume wakati wa Kampeni za uchaguzi na uchaguzi.

Kifungu cha 124A (2) (a) na (b) kinasema Maadili hayo yatakubaliwa na kufuatwa na kila chama cha siasa na mgombea wa nafasi yoyote atapaswa kusaini Fomu namba 10 ya kukubali, kuyaheshimu na kutekeleza Maadili ya Uchaguzi ya mwaka 2015, ambapo Wagombea wote walisaini kwani ilikuwa ni mojawapo wa kigezo cha kuteuliwa kuwa mgombea wa nafasi ya Rais /Makamu wa Rais, Mbunge au Diwani.

Katika Maadili ya Uchaguzi ya mwaka 2015 yaliyokubaliwa na kusainiwa na vyama vyote vya Siasa tarehe 27 Julai, 2015, vyama vyote vilikubali kuheshimu na kutekeleza Maadili hayo na ukiukwaji wowote wa Maadili hayo utashughulikiwa kwa mujibu wa kipengele cha 5.11 cha Maadili hayo.

Hivi karibuni kumejitokeza baadhi ya vyama vya siasa kuanza kufanya mikusanyiko ya Kampeni ya Rais. Mikusanyiko hiyo yenye sura ya Kampeni haipo katika Ratiba ya Kampeni ya Urais. Mikusanyiko hiyo yenye sura ya kampeni inaweza kuingiliana na ratiba za kampeni za chama kingine katika maeneo husika na hivyo kusababisha uvunjifu wa amani.

Iwapo Chama cha Siasa kinachotaka kufanya mikusanyiko yenye sura ya Kampeni za Uchaguzi kinapaswa kuwasilisha mapendekezo yake kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi ili aweze kuitisha Kamati ya Ratiba ya Kampeni ya Rais inayojumuisha vyama vyenye Wagombea wa Kiti cha Rais ambavyo kwa mujibu wa kanuni tajwa hapo juu, vinaweza kukubali au kukataa mapendekezo hayo.

Vyama vyote vya Siasa vizingatie Ratiba ya Kampeni ya Uchaguzi wa Rais na viache kufanya mikusanyiko ya aina yoyote ambayo haipo katika Ratiba ya Kampeni ya Rais.

Chama kitakachokiuka maelezo haya kitakuwa kimekiuka kipengele cha 2.1. (a) cha Maadili ambacho kinaelekeza kuwa ni wajibu wa vyama vya siasa na Wagombea kuheshimu na kutekeleza Sheria za Uchaguzi, Kanuni za Uchaguzi, Maadili ya Uchaguzi na Maelekezo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi pamoja na Sheria zingine za nchi katika kipindi chote cha Uchaguzi.

Ukiukwaji wa Maadili ya Uchaguzi adhabu zake zimefafanuliwa katika kipengele cha 5.10 na 5.12 cha Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015.

Imetolewa na:

Kailima, R.K
MKURUGENZI WA UCHAGUZI
Tarehe 25 Agosti, 2015


No comments:

Post a Comment