Saturday, April 26, 2014

MAAJABU: AKUTWA NA DHAHABU VIPANDE 12 TUMBONI KWAKE


Jopo la madaktari wapasuaji walipigwa na mshangao pale ambapo hawakutegemea wangekuta utajiri ndani ya tumbo la mgonjwa aliyelalamika kuwa na maumivu makali ya tumbo baada ya upasuaji.

Mgonjwa huyo ambaye jina lake halikutajwa, alikuwa, alificha vipande 12 vya dhahabu tumboni mwake ili kuingiza dhahabu hiyo nchini India kwa njia hiyo ili kukwepa kodi, ripoti ya polisi na madaktari ilieleza jumanne iliyopita.

Kwa mujibu wa CNN India, kila kipande kina uzito wa gramu 33, alisema C.S. Ramachandran, ambaye ndie aliongoza jopo la madaktari katika upasuaji huo kwenye hospitali iliyoko jijini New Delhi tarehe 9 Aprili mwaka huu.

ANGALIA PICHA ZAIDI ZA XRAY. . .

Mgonjwa huyo mwenye umri wa miaka 63, raia wa India, alifika hospitali siku moja kabla ya operesheni, akilalamika kuwa na maumivu makali sana ya tumbo yanayo ambatana na kichefuchefu.

“Alituambia kwa bahati mbaya alimeza kifuniko cha chupa ya plastiki,” alisema Ramachandran.

Hata baada ya kufanyiwa uchunguzi, hawakuweza kugundua hilo mara moja. “Hatukutegemea kuwa ni vipande vya dhahabu” alisema Daktari. “Lakini ndio hivyo, X-Ray ilionesha kuna vitu vimeziba utumbo, ambapo ilihitajika upasuaji kuondoa.”

Siku ya operesheni yake, madaktari walipigwa na butwaa walipotoa vipande vya njano vya chuma kutoka tumboni.

“Halikuwa jambo la kutegemea” Ramachandran alisema. Uongozi wa hospitali hiyo ulikabidhi vipande hivyo vya dhahabu kwa polisi. Vipande hivyo vilipelekwa idara ya ushuru, ambapo wanafanya uchunguzi zaidi, alisema Alok Kumar, Kamishna wa Polisi.

Hakutaka kutaja jina la mgonjwa huyo, na wala hakusema dhahabu hiyo imeingizwa kutoka nchi gani. Hata hivyo mgonjwa huyo aliruhusiwa kutoka hospitali na inasemekana anaendelea vizuri.

India ndio soko la pili kubwa la dhahabu duniani ambapo China ndio inaongoza, hiyo ni kwa mujibu wa Baraza la Dhahabu Duniani (World Gold Council). Imeelezwa kuwa India imeongeza rekodi yake ya kuingiza vipande vya dhahabu kwa asilimia 16 kwa mwaka jana (2013) ambapo kodi hutozwa asilimia 10 ya thamani kwa kipande.



No comments:

Post a Comment