Tuesday, March 18, 2014

WAZEE WA YANGA WAWEKA "SILAHA" CHINI…WAKUBALI YAISHE

Dar Es Salaam

Wazee wa Klabu ya Yanga jijini Dar es Salaam, wametoa tamko la kusitisha maandamano yao ambayo walikuwa wamepanga yafanyike kushinikiza serikali kutoa kibali cha ujenzi wa uwanja wao wa kisasa unaotarajia kujengwa Jangwani, Dar es Salaam.

Tamko la kusitisha maandamano limetolewa Dar es Salaam leo baada ya baadhi ya viongozi wa juu wa timu hiyo kukutana na viongozi wa serikali. Viongozi wa serikali walitoa tamko kuhusu kushughulikia ombi lao hali iliyosababisha viongozi wa Yanga kusitisha maandamano waliyopanga kuyafanya.

Wiki iliyopita Katibu wa Baraza la Wazee wa Yanga, Ibrahim Akilimali alitoa siku tano kwa Baraza la Madiwani Manispaa ya Ilala liwe limewapa kibali cha ujenzi huo, vinginevyo waliahidi kufanya maandamano makubwa.

Akizungumza na Immamatukio jijini Dar es Salaam leo, Akilimali alisema wamesitisha kuandamana mara baada ya viongozi wa serikali kuwataka watulie kwa kuwa ombi lao linashughulikiwa.
Alisema juzi viongozi wa juu wa klabu hiyo walikutana na viongozi wa serikali akiwepo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sadik Mecky Sadik, Meya wa Ilala Jery Silaa na Diwani wa Kata ya Jangwani ambapo walikubaliana ombi lao lifanyiwe kazi.

Akilima alisema serikali kupitia Manispaa ya Ilala ilieleza kuwa ombi lao linashughulikiwa kwa haraka, hivyo aliwataka wanachama wa klabu hiyo kuelewa jambo hilo bila kuwepo na migogoro.

Aliweka wazi kuwa wanaamini serikali kupitia Manspaa ya Ilala watalishughulikia ombi lao, ingawa alisisitiza kuwa ikitokea ombi lao hilo linaloshughulikiwa likija na majibu ya hapana itatafuta mbinu nyingine.

"Sisi tumeomba hivyo majibu ni mawili ndiyo tumepata au tumekosa, ikitokea likaja jibu la kukosa hapo ndiyo kutakuwa na utata na kuamua cha kufanya," alisema.

Aliongezea kuwa klabu hiyo imejiandaa kuwalipa watu waliongezeka katika eneo lao, hivyo hawaoni sababu za kwenda kujenga nje ya mjini wakati wao ni watoto wa mjini.

No comments:

Post a Comment