Monday, February 03, 2014

WANAUME 28 WATAIRIWA KINGUVU NA DAKTARI FEKI SEBULENI

Hai

Daktari bandia na mkazi wa kijiji cha Mudio kata ya Masama Mashariki,wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, Athuman Kimaro, amewafanyia tohara kwa nguvu wanaume 28 wa kijiji hicho na kutishia afya zao ikiwamo kupata ugonjwa wa Ukimwi.

Daktari huyo bandia amekuwa akiwafanyia tohara hiyo wateja wake katika sebule ya moja ya nyumba kijijini humo huku pia akitumia majiko ya mkaa na kuni kwa ajili ya kuchemshia vifaa anavyovitumia kwa ajili ya kazi hiyo.

Mganga mkuu wa wilaya ya Hai Dk Paul Chaote amethibitisha kuwapo kwa daktari huyo aliyedai anafanyakazi katika hospitali ya Mount Meru mkoani Arusha ingawa taarifa hizo hazijathibitishwa na hospitali husika licha ya kuulizwa.

Hata hivyo tayari serikali imesimamisha zoezi la tohara hiyo huku pia daktari huyo bandia akishikiliwa na jeshi la polisi kwa ajili ya mahojiano zaidi kuhusu taaluma yake na uhalali wa zoezi hilo.

Aidha Dk Chaote alisema kuwa uchunguzi wa awali pia umebaini kwamba daktari huyo bandia amekuwa akiwatibu wagonjwa wake hao kwa kutumia duka lake la dawa lililopo kijijini humo licha ya kwamba halitambuliki lakini pia mhudumu wake akikosa sifa za kufanya kazi hiyo.

“Tulipata taarifa kuhusu kufanyika kwa tohara kwa wanaume wa kijiji cha Modio na baada ya kufuatilia tulibaini ni kweli na tulipomhoji Kimaro alidai ni daktari msaidizi katika hospitali ya Mount Meru Arusha, tunamhoji kwa ajili ya taarifa zaidi”alisema.

Alisema baada ya taarifa za tukio hilo walifuatilia kijijini hapo kwa kushirikiana na jeshi la polisi na kubaini nyumba na vifaa vilivyokuwa vikitumika havikubaliki kiafya lakini pia duka la dawa ambazo wanapewa wagonjwa baada ya kufanyiwa tohara linaendeshwa kinyume cha taratibu.

"Tumeanza uchunguzi ili kuwapata watu waliofanyiwa tohara ili kujua wanaendeleaje kiafya, hii ni kutokana na aina huduma waliyopata haikubali kiafya”alisema.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Masama Mashariki, Ally Mwanga alikiri kuwapo kwa tukio hilo alilodai limesababisha usumbufu kwa wananchi wake huku wengine wakishindwa kwenda katika shughuli za uzalishaji mali kwa hofu ya kukamatwa ili kufanyiwa tohara.

Mwanga alisema alipokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi juu ya kufanyika kwa vitendo hivyo jambo ambalo alitoa taarifa polisi wilayani Hai ambapo baadaye uchunguzi ulifanyika na mhusika pamoja na timu yake kukamatwa.

No comments:

Post a Comment