Miili ya askari watano wa jeshi la polisi mkoa wa Dodoma waliofariki kwa ajali ya gari juzi,jana iliagwa na kusafirishwa kuelekea nyumbani kwao.
Akizungumza na waombolezaji katika ibada ya kuaga miili hiyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma David Misime alimtaka kila mmoja kutumia utashi aliopewa na Mungu katika kupunguza ajali za barabarani ikiwa ni pamoja na kuwa mabalozi kwa kila mmoja kwa kuwakumbusha kufuata sheria za usalama barabarani ili kuweza kuepuka ajali hizo.
“Wakati mwingine sisi ndio tunazitafuta ajali kwa kukiuka sheria za usalama barabarani na tutumie utashi tuliopewa na Mungu kupunguza tatizo hili lakini pia tusimsingizie Mungu kutokana na ajali hizi wakati ni makosa yetu wenyewe”alisema Misime.
Aidha aliwataka ndugu wa marehemu hao kutowanyanyasa wajane wa marehemu hasa kugombea mali za marehemu kwani kumekuwa na tabia ya baadhi ya watu kuingilia mali za marehemu kwa kutaka kuzimiliki wenyewe huku mke ama mume wa marehemu akiachwa bila kitu huku wengine wakiwa na watoto ambao bado wanahitaji kusomeshwa na kulelewa katika malezi bora.
Akisoma wasifu wa marehemu hao Mrakibu wa polisi(SP) Joshua Mwafilango alisema kuwa askari hao walikuwa tegemezi kubwa kwa jeshi hilo kwa elimu na ngazi walizokuwa nazo ambao wengine wamefariki wakiwa hawajatimiza miaka mitatu tangu waanze kazi na kuongeza kuwa mchango wao na nguvu bado vilikuwa vinahitajika.
Naye Mchungaji kiongozi wa kanisa kuu la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika Japhet Sudayi aliwataka wananchi waliofika katika ibada hiyo kujiandaa kwa kumuamini mungu wao kwa kutotenda maovu ili kila mmoja awe tayari kiroho na hata kimwili.
Askari hao walifariki papohapo usiku wa kuamkia tarehe 01/02/2014 kwa ajali ya gari ndogo lenye namba za usajili T.770 ABT aina ya Toyota Corolla lililogongana na basi la Mohamed Trans lenye namba T.997 AVW aina ya Scania basi katika eneo la Mtumba manispaa ya Dodoma lililokuwa likitokea jijini Dar es salaam ambapo askari hao walikuwa wakitokea katika sherehe ya kuuaga mwaka2013 na kuukaribisha mwaka2014 pamoja na kuwaaga Maofisa,wakaguzi na askari mbalimbali wastaafu wa jeshi hilo.
Marehemu Evarist Bukombe alizaliwa mwaka 1980 katika kijiji cha Kizazi Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma na alisafirishwa kwenda Kigoma,Jackline Tesha alizaliwa mwaka 1991 Kijiji cha Shimbwe wilaya ya Moshi vijijini na kusafirishwa kwenda Kilimanjaro,Jema Luvinga alizaliwa mwaka 1994 katika kijiji cha Lugalo wilaya ya Kololo mkoani Iringa na kusafirishwa kwenda mkoani huko,Deogratius Mahinyila alizaliwa mwaka 1985 wilayani Mpwapwa nasafirishwa kwenda Wilayani huko na Adolf Silla alizaliwa mwaka 1963 katika kijiji cha Mlanga ‘W’ kilichopo wilaya ya Kongwa mkoani hapa na mwili wake kusafirishwa kwenda wilayani huko.
Ibada hiyo ilihudhuliwa na viongozi mbalimbali wa dini na serikali,wafanyabiashara,madereva wa pikipiki na magari pamoja na makundi mengine ya watu ambao wote kwa pamoja walitoa salamu za rambirambi kwa ndugu wa marehemu.
No comments:
Post a Comment