Chunya
Wakimbizi na jamii ya Waarabu kutokea mikoa ya Kigoma na
Tabora wamedaiwa kuvamia pori la Akiba la Piti lililopo kata ya Mafyeko
wilayani Chunya na kuua jumla ya tembo 20.
Pori la Piti lipo mpakani mwa wilaya za Sikonge mkoani Tabora
na Manyoni mkoani Singida. Akizungumza
na waandishi wa habari waliotembelea wilayani humo mwishoni mwa wiki Kaimu
Ofisa Wanyamapori wa wilaya ya Chunya Abdallah Mgonja alisema kuwa Tembo
13 waliuawa kwa kupigwa risasi na mizoga yao kutelekezwa porini.
Alisema walibaini kutumika kwa wakimbizi katika ujangiri huo
baada ya kuokota bunduki ya kivita aina ya SGM ambayo inatumika na wakimbizi wa
nchi jirani ambao hutumiwa na waarabu kufanya ujangiri huo.
Alisema katika operesheni hiyo ya 2012-’13 maofisa
wanyamapori waliokota meno 6 ambapo majangiri walikimbia na kwamba asilimia
kubwa ya majangiri wanaovamia eneo hilo ni wakimbizi wanaotumiwa na Waarabu
wanatokea mikoa ya jirani ya Tabora na Kigoma.
Bw.Mgonja alisema kuwa eneo hilo la Pori la Akiba la Piti
ambalo awali lilikuwa pori la wazi kabla ya kupandishwa daraja limekuwa
likivamiwa mara kwa mara na majangiri ambao makao makuu yao yapo katika kata ya
Kitunda, Sikonge na Mafyeko. ‘’Mwishoni
mwa mwaka jana tumekuta mizoga ya Tembo watatu,Twiga wawili waliouawa na
kukatwa vichwa,
Nyati watano, Swala 6, pia tulikamata bunduki aina ya SMG
inayotumiwa vitani, hawa wanategwa kwa nyaya na kuuawa kwa magobole’’alisema
Bw. Mgonja. Alisema kuwa hadi sasa kesi
tatu zinazohusiana na ujangiri zimefikishwa mahakamani ambapo kati ya hizo kesi
mbili zinahusu Pembe za Ndovu.
Bw. Mgonja alisema kuwa wilaya hiyo ina aina zote za wanyama
wanaopatikana katika maeneo mengine ya hifadhi za Katavi na Ruaha isipokuwa
wanyama aina ya Faru na Nyumbu.
Wilaya ya Chunya ina jumla ya mapori ya akiba mawili ya Piti
na Lukwati na pori la wazi la Rungwa ambalo lipo upande wa Chunya na sehemu ya
Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na kwamba kuna jumla ya vitalu 9 na makampuni 7
ambayo yanaendesha uwindaji wa kitalii.

No comments:
Post a Comment