TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein,(katikati) na viongozi mbali mbali walioshiriki matembezi ya Bonanza ya 5 ya vikundi vya mazoezi ya viungo, yaliyoanzia uwanja wa Kisonge hadi uwanja wa Amaan, Wilaya ya Mjini Unguja
Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wananchi
kujenga na kuendeleza utamaduni wa kufanya mazoezi ili kuimarisha afya zao
pamoja na kujikinga na maradhi yanayoweza kuepukika.
Dk. Shein ametoa
kauli hiyo leo wakati alipokuwa akizungumza na wanachama wa klabu za mazoezi na
vyama vya michezo katika Bonanza Maalum la Mazoezi ya Viungo lililofanyika
katika uwanja wa Amaan mjini Unguja.
Kabla ya kuzungumza
na wanamichezo hao Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi akiwa
amefuatana na Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili
wa Rais Balozi Seif Ali Iddi pamoja na viongozi wengine walishiriki matembezi
ikiwa ni sehemu ya Bonanza hilo yaliyoanzia Michenzani mjini Unguja hadi Uwanjani
hapo.
Dk. Shein aliwaeleza
washiriki kuwa ni jambo lililo dhahiri kuwa kufanya mazoezi ni jambo la msingi
sana katika kuimarisha afya ya mwili na kuchangamsha akili hivyo Serikali ina
kila sababu ya kuziunga mkono jitihada walizozianzisha za kuunda vikundi vya
mazoezi.
Alifafanua kuwa
hivi sasa kumekuwepo na maradhi mengi ambayo hapa kwetu yanaelezwa kusababishwa
na mabadiliko ya mtindo wa maisha na kuyataja maradhi hayo kuwa ni pamoja na
shinikizo la damu, kisukari na kuongezeka unene ambayo yanaweza kupunguza kwa
kufanya mazoezi.
Hata hivyo pamoja
na ukweli huo alibainisha kuwa kuimarika kwa huduma za afya na huduma hizo
kusogezwa karibu na wananchi kumerahisisha wananchi kugundua maradhi mengi kuliko
iliyokuwa huko nyuma.
Dk. Shein aliwahakikishia
wanamichezo nchini kuwa Serikali ya Awamu ya Saba itaendelea jitihada zilizoanzishwa
na Serikali za awamu zilizopita kuimarisha michezo ikiwemo kuweka mazingira na
miundombinu bora ya michezo.
Kwa hiyo
aliwapongeza Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo kwa kutekeleza
maagizo yake kikamilifu ya kubadili haiba ya uwanja wa michezo vya Amaan Unguja
kwa wakati pamoja na kualika timu za nje katika mashindano ya kikombe cha
Mapinduzi mwaka huu.
Aliongeza katika
kuimarisha michezo Serikali imeuwekea pia nyasi bandia uwanja wa Michezo wa
Gombani Pemba na huduma nyingine ili kukidhi viwango vya kimataifa. Kuhusu
uwanja wa Mao Dk. Shein alisema tayari Serikali imeshatiliana saini makubaliano
na Serikali ya China kuujenga upya uwanja huo.
Sambamba na pongezi
hizo alieleza kufurahishwa na Wizara hiyo kuhamasisha michezo mijini na
vijijini huku akitolea mfano ushiriki wa vikundi kutoka sehemu zote za Zanzibar
pamoja na Tanzania Bara katika Bonanza la mwaka huu.
Wakati huo huo Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameunga
mkono tamko la Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo la kuifanya siku ya
tarehe 01 Januari kila mwaka kuwa siku ya mazoezi kitaifa na ametaka maandalizi
ya Bonanza hilo ambalo litakuwa la Sita yafanyike kwa umakini mkubwa.
Akizungumza kumkaribisha
Mgeni Rasmi, Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk
alisema Bonanza hilo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Mheshimiwa Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi la kuitaka Wizara hiyo kurejesha hamasa ya
wananchi kupenda nchini.
Kufuatia agizo hilo
alibainisha Waziri huyo wa Michezo kuwa Serikali imeamua siku ya tarehe 01
Januari ya kila mwaka iwe siku ya mazoezi kitaifa ambapo kila mwananchi popote
alipo nchini atashiriki mazoezi.
Aliongeza kuwa
Bonanza hilo la Tano la Mazoezi ambalo limejumuisha vikundi vya mazoezi 65 kutoka
Unguja, Pemba na Tanzania Bara badala ya 50 vilivyapangwa awali ni ishara ya wananchi
kuitikia wito wa kufanya mazoezi pamoja na kuimarika uongozi wa ZABESA.
Kwa hiyo aliahidi kushirikisha
vikundi kutoka sehemu nyingi zaidi ya nchi katika bonanza lijalo kuongeza
hamasa na pia kuimarisha vikundi vya mazoezi.
Kwa uapande wake
Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Zanzibar Sharifa Khamis alieleza kuwa Bonanza
hilo ni uzinduzi wa Vuguvugu la Miaka 50 ya Mapinduzi kwa wanamichezo ambalo litaendelea
hadi tarehe 13 Januari mashindano hayo yatakapofikia fainali.
Amewashukuru wadau
mbalimbali waliofanikisha Bonanza hilo pamoja na michezo itakayofanyika wakati
wa maadhimisho hayo. Amezitaja nchi za nje zilizoleta timu kuwa ni pamoja na Kenya,
Uganda, Zambia, Sudan Kusini na Ghana.
Katika risala yao iliyosomwa na Mjumbe wa Kamati ya
Utendaji ya Chama cha Wafanya Mazoezi ya Viungo Zanzibar- ZABESA bibi Hawa
Abdalla Mandred wanamazoezi hao waliiomba Serikali ifanye tathmini ya kiafya kwa
wanamazoezi hao na Serikali kufanyia kazi matokeo ya tathmini yake kwa faida ya
wanamazoezi na kwa Taifa kwa jumla.
Risala hiyo ilizidi
kueleza kuwa wanamazoezi hivi sasa wanazidi kuhamasisha wananchi wengine zaidi
kujiunga na vyama vya mazoezi na takwimu za kila mwaka zimekuwa zikionesha kuwa
idadi ya vikundi na wanachama wa vyama vya hivyo imekuwa ikiongezeka kila mwaka.
Sambamba na
ongezeko hilo jambo muhimu la kutia moyo alisema Bi Hawa ni kuona kuwa kumekuwa
na ongezeko kubwa la wanamazoezi wanawake tofauti na miaka mitano iliyopita
lilipoanzishwa bonanza hilo.
Alisema ZABESA inaamini
kuwa kazi hiyo ya kuhamasisha mazoezi inalisaidia Taifa kwa kuwa mazoezi hayo
yanasaidia kuepusha maradhi yasiyo ya lazima na pia hata kutibu baadhi ya mardhi
bila ya mwananchi kupaswa kweda hospitali hivyo kulipunguzia Taifa gharama za
matibabu.
No comments:
Post a Comment