Mgombea udiwani kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) katika uchaguzi mdogo kata ya Nyasura Jimbo la Bunda mkoani Mara amepata pingamizi toka kwa mgombea mwenzake kwa tiketi ya Chama cha NCCR-Mageuzi Acetic Maragila.
Maragila amempinga mgombea huyo wa CHADEMA kuwa jina analotumia la Wassira si jina lake halisi. Amedai mgombea huyo wa CHADEMA ametumia jina la Julius Magambo Wassira badala ya jina lake halisi la Julius Webiro Magambo.
“ jina halisi la mgombea wa CHADEMA ni Julius Webiro Magambo na siyo Julius Magambo Wasira kama fomu zinavyoonesha anatumia jina la wasira ili apate umaarufu kupitia kwa waziri wa Nchi ofisi ya Rais(Mahusiano na Uratibu),Stephen Wasira”ilisema sehemu ya barua hiyo ya pingamizi.
Mtafaruku ilitoka wakati Msimamizi msaidizi wa uchaguzi kata ya Nyasura , John Yapanda kunusurika kupigwa na wanachama wa CHADEMA baada ya kufika kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni wa chama hicho iliyoanza jana akimtaka mgombea huyo wa CHADEMA ajibu pingamizi lililokuwa limewekwa dhidi yake.
Tukio hilo lilitokea saa 9.50 alasiri baada ya Yapanda ambaye ni ofisa mtendaji wa kata hiyo kufika kwenye eneo la mkutano huo uliokuwa ukifanyika katika viwanja vya Nyasura Senta akimtaka Magambo Wasira asaini pingamizi kama ishara ya kulipokea.
Hata hivyo Yapanda hakufanikiwa kumfikishia mgombea huyo kitabu hicho baada ya kuzongwa na viongozi waandamizi wa chama hicho waliokuwepo mahala hapo wakimtaka aueleze umma nini kimemleta huku wengine wakianza kumvuta shati kuashiria kichapo.
Hata hivyo alifanikiwa kufika jukwaani ambapo baada ya kutoa maelezo yaliamsha hasira miongoni mwa wafuasi wa CHADEMA kwa lengo la kumwadhibu msimamizi huyo wakimtuhumu kuwa ametumwa na CCM.
Hata hivyo Katibu cha wa CHADEMA wilaya ya Bunda Samuel Imanani alifanikiwa kutuliza ghasia hizo kwa kutoa nakala ya kitambulisho cha mpiga kura cha mgombea huyo kama uthibitisho wa jina lake huku wakimtaka awe makini na pingamizi anazoletewa.
Akizungumzia hali hiyo mwenyekiti wa CHADEMA mkoani Mara Charles Kanyere alisema ni njama za chama tawala za kumdhoofisha kifikira mgombea wao na kuwataka wafuasi wa chama hicho kujihadhari huku akimwelezea msimamizi huyo kuwa mwadilifu anayelitafutia kila jambo ukweli wake.
Hata hivyo wengi wilayani Bunda wametoa maoni yao juu ya jina la Wassira linavyotumiwa na wanasiasa chipukizi kutoka ukoo wa Wassira kwa kuhusisha jina hilo na lile la Mbunge wa jimbo hilo Stephen Masato Wassira huku wakieleza kuwa hilo ni jina la ukoo na kwamba sio kila anayetumia jina hilo ni motto wa Mbunge Wassira.
Wameleeza kuwa mgombea huyo na wengine ambao mara nyingi wanatoka katika ukoo wa Wassira wamekuwa wakipotosha umma kwa kujipambanua kuwa ni watoto wa mbunge Stephen Masato Wassira kwa lengo la kupata umaarufu kisiasa.
No comments:
Post a Comment