Tuesday, January 14, 2014

HATIMAYE OYSTERBAY POLISI KUUZWA YAONGELEWA NA WIZARA


TAARIFA YA WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI ILIYOTOLEWA NA MSEMAJI WA WIZARA ISAAC J. NANTANGA KATIKA MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI TAREHE 14 NOVEMBA, 2012 KUHUSU MRADI WA UWEKEZAJI KATIKA ENEO LA OYSTERBAY POLISI, MANISPAA YA KINONDONI, DAR ES SALAAM
Madhumuni ya kikao hiki ni kutaka kuufahamisha Umma kuhusu Mradi wa Uwekezaji ambao unategemewa kuendeshwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Polisi, katika eneo la Polisi Oysterbay lililopo katika Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Chimbuko la Mradi huu hasa linatokana na tatizo kubwa la uhaba wa makazi ya askari Polisi linaloikabili Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Katika kukabiliana na tatizo hili, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imekuwa ikibuni mbinu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuishirikisha Sekta binafsi katika ujenzi wa nyumba za Polisi, chini ya Dhana ya Ushirikiano wa Sekta ya Umma na Sekta Binafsi.

Mfano mmojawapo ni ule wa nyumba za Polisi Kilwa Road ambapo Shirika la NSSF lilishiriki katika kufanikisha mradi wa ujenzi wa nyumba hizo kwa mkataba na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Kutokana na mahitaji ya nyumba za Polisi ambayo yanakadiriwa kufikia nyumba 34,710, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ilibaini kuwa eneo lake la Polisi Oysterbay lenye ukubwa wa ekari 24 linaweza kutumiwa kwa uwekezaji wa majengo mbalimbali ambayo yataliwezesha Jeshi la Polisi kupunguza tatizo la ukosefu wa makazi ya askari na pia kupata mapato endelevu kutokana na tozo la majengo hayo.

SOMA ZAIDI...


Ili kufanikisha azma hiyo, Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia Jeshi la Polisi, na kwa kuzingatia Kanuni ya Manunuzi Na. 74(4), ilitafuta Mshauri Mwelekezi kwa ajili ya kufanya uchambuzi yakinifu ili kujiridhisha kama mradi huo utakuwa na faida, na Mshauri aliyepatikana ni Bureau for Industrial Cooperation (BICO) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Mshauri huyu aliteuliwa kutokana na uzoefu na utekelezaji wa mradi wa Mlimani City wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Baada ya uchambuzi yakinifu kukamilika mwezi Novemba, 2011 na kuonekana kuwa Mradi huo una faida, zabuni ya Uwekezaji ilitangazwa tarehe 9 Novemba, 2011 na tarehe 14 Novemba, 2011. Matangazo haya yalikuwa ya Kimataifa (International Tendering).
Baada ya Matangazo haya kutolewa, Kampuni kumi (10) zilileta maombi na kununua nyaraka maalumu za kujieleza kuhusu maombi hayo. Hata hivyo ni kampuni mbili tu ambazo zilirejesha nyaraka hizo na kampuni hizo ni Mara Capital Group Ltd ya nchini Uganda na Quality Group Ltd. ya hapa nchini.
Nyaraka za kampuni hizo zilifunguliwa tarehe 23 Desemba 2011 na baada ya mapitio yaliyoshirikisha wataalamu toka BICO, Jeshi la Magereza pamoja na Jeshi la Polisi, Kampuni ya Mara Group Ltd. ya Uganda ilishinda.
Kampuni nyingine ambazo zilikuwa zimechukua nyaraka za maombi ni:
  • Orbit Developers Ltd
  • China Road & Bridge Corporation
  • Standard Real Estates International
  • Phoenix Of Tanzania Assurance Co. Ltd
  • Hab Consultant
  • Webb Uronu & Partners Ltd
  • Cover Drive Limited
  • Turkish Embassy
Mkataba wa Awali kati ya Wizara ya Mambo ya Ndani na Mara Group ulisainiwa tarehe 23 Juni, 2012 na baada ya mambo yote kukamilika, Kampuni ya Mara Group Ltd. itapaswa kuwekeza katika maeneo yafuatayo:
1.Maduka Makubwa (Shopping Malls)
2.Hospitali kubwa ya kisasa
3.Ukumbi wa Mikutano
4.Hoteli
5.Ofisi za kukodisha
6.Makazi ya kukodisha
7.Maeneo ya maegesho ya magari
Kufuatana na mkataba wa awali, Mwekezaji huyo itabidi ajenge makazi mapya ya wakazi wa Oysterbay Polisi katika eneo la Mikocheni, (nyumba 20), na Kunduchi, (nyumba 330), pamoja na Ofisi ya kisasa ya Polisi palepale katika eneo la Oysterbay Polisi.
Jumla ya gharama za Mradi ni USD 270 milioni, karibu sawa na shilingi bilioni 426.6 za Kitanzania. Kati ya hizo USD 250 (Tsh. Bilioni 395) zitakuwa kwa ajili ya uwekezaji wa majengo ya biashara na USD 20 milioni (Tsh. Bilioni 31.6) zitatumika kujenga makazi ya Polisi na Kituo cha kisasa cha Polisi Oysterbay.
Kufuatana na Mkataba wa Awali wa Uwekezaji huu, ardhi katika eneo la uwekezaji inabaki kuwa mali ya Serikali na majengo yatakayojengwa yatakuwa mali ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ambapo Mwekezaji atakuwa ni mpangaji tu.
Mwekezaji wa Mradi huu amekubali kulipia utumiaji wa ardhi na majengo hayo kwa tozo la USD. 2.76 milioni (TZS 4.36 Bilioni) kwa mwaka, mara tu ya baada ya kukamilika kwa ujenzi na mradi kuanza, lakini tozo kamili litajulikana baada ya kufanya uchambuzi wa kibiashara na kupitishwa na Bodi Kasimu ya Jeshi la Polisi. Aidha tozo hili litabadilika kulingana na hali ya uchumi itakavyokuwa inabadilika.
Kwa mujibu wa makubaliano ya awali, mwekezaji anatarajiwa kutumia miezi kumi na moja kukamilisha michoro na uchambuzi wa mazingira na mradi unatarajiwa kuanza mwezi Julai, 2013 baada ya kusaini mkataba.
Mradi huu utaanza na kujengwa kwa makazi ya askari ya nyumba 350 kama ilivyoelezwa hapo awali na pia kituo cha Polisi cha kisasa katika eneo hilo la Oysterbay ili kuweza kuwahamisha askari waliopo katika eneo hilo na kisha majengo mengine yatafuata.
Aidha muda wa uendeshaji wa Mradi utakuwa wa miaka 50 na baada ya muda huo, Serikali itakuwa na haki ya kuamua ni jinsi gani mradi huo uendelee.
Manufaa ya Mradi huu ni kama ifuatavyo:
  1. Ujenzi wa Mradi utatoa ajira mbalimbali kwa wananchi.
  2. Eneo la Mradi litabaki kuwa mali ya Serikali na majengo yote yatakayojengwa katika eneo hilo yatakuwa pia ni mali ya Serikali na Mwekezaji atabaki kuwa mpangaji tu.
  3. Tozo la USD zisizopungua 2.76 (Tsh. 4.36 bilioni) litapatikana kila mwaka na hivyo kulisaidia Jeshi la Polisi kufanya shughuli nyingine za maendeleo.
  4. Kituo cha kisasa kitajengwa katika eneo la Mradi na hivyo kusaidia kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi.
  5. Mwekezaji atajenga nyumba za makazi za familia 350 katika eneo la Mikocheni (nyumba 20) na Kunduchi (nyumba 330), ingawaje gharama ya nyumba hizi itakatwa kutokana na tozo atakalokuwa anatoa Mwekezaji.
  6. Serikali itapata kodi kutokana na shughuli mbalimbali za kibiashara zitakazokuwa zinaendeshwa katika eneo hilo.
  7. Wananchi watapata huduma mbalimbali zitakazokuwa zinatolewa katika eneo la Mradi.
MWISHO
- See more at: http://www.moha.go.tz/index.php/82-news-and-events/188-taarifa-ya-wizara-ya-mambo-ya-ndani-ya-nchi-iliyotolewa-na-msemaji-wa-wizara-isaac-j-nantanga-katika-mkutano-na-waandishi-wa-habari-tarehe-14-novemba-2012-kuhusu-mradi-wa-uwekezaji-katika-eneo-la-oysterbay-polisi-manispaa-ya-kinondoni-dar-es-salaam#sthash.VT3W39vt.WJGixQeB.dpuf

No comments:

Post a Comment