Shinyanga
Katika
hali isiyokuwa ya kawaida mfanyakazi mmoja wa kampuni ya simu za mkononi ya
TIGO mkoani Shinyanga amekufa papo hapo baada ya kudaiwa kunywa pombe nyingi
aina ya Konyangi kupita kiasi.
Kwa
mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo wamemtaja mfanyakazi huyo kuwa ni Godi
Mangala (34) aliyekuwa akiishi mtaa wa Majengo mapya kata ya Ngokolo manispaa
ya Shinyanga ambalo limetokea juzi saa moja usiku wakati wa sikukuu ya
krismasi.
Mashuhuda
hao wamewaeleza waandishi wa habari mjini kwamba siku hiyo ya tukio, Godi akiwa
na marafiki zake katika moja ya glosari za mjini humo waliamua kupata vinywaji
ambapo waliamua kunywa pombe hiyo kwa kushindana ili kuweza kumpata bingwa wa
utumiaji wa kilevi hicho.
Walisema
muda mfupi baada ya marehemu kuonesha ubingwa wake katika unywaji wa pombe hiyo
alionesha dalili za kuzidiwa na kuishiwa nguvu hali ambayo ilisababisha rafiki
zake wamtafutie usafiri na kumrudisha nyumbani kwake ili apumzike.
“Hata
hivyo tulipoona hali yake inaendelea kuwa mbaya tulichukua uamuzi wa kumkimbiza
katika hospitali ya serikali mkoani Shinyanga ili aweze kupatiwa matibabu
haraka lakini hata hivyo alifariki dunia kabla ya kufikishwa hospitali,”
alieleza mmoja wa marafiki wa marehemu ambaye hata hivyo hakupenda kutajwa jina
gazetini.
Kwa
upande wake John Maganya ambaye pia ni mmoja wa marafiki wa marehemu alielezea
kushitushwa kwake na tukio hilo ambalo limesababisha kifo cha rafiki yake
ambaye hata hivyo alisema enzi za uhai alikuwa ni mzoefu katika unywaji wa
pombe japokuwa kuna wakati alikuwa akizimia na kuzinduka.
“Nimeshitushwa
na kifo cha rafiki yangu, kwani kama ni pombe mbona alikuwa mzoefu, nafikiri
hii Konyagi aliyokuwa anakunywa na wenzake imesababisha kifo chake, maana
tumeelezwa kwamba alikunywa mizinga mitano kwa mkupuo, ni hatari,” alieleza
Maganya.
Kwa
upande wake mganga mfawidhi katika hospitali ya serikali mkoani Shinyanga, Dkt.
Fredrick Mlekwa alikiri kupokea mwili wa marehemu huyo juzi mnamo saa moja
usiku na kwamba baada ya kuchunguzwa na kubainika tayari ameishafariki
alielekeza mwili huo ukahifadhiwe katika chumba cha kuhifadhia maiti
hospitalini hapo.
Kwa
upande wake Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Evarist Mangala alisema
hakuwa na taarifa juu ya tukio hilo na kwamba huenda ndugu wa marehemu
hawakuona umuhimu wa kutoa taarifa polisi ya kifo cha ndugu yao.
Kwa
mujibu wa taarifa zilizopatikana jana mjini hapa, tayari ndugu wa marehemu
waliuchukua mwili wake na kupelekwa jijini Mwanza eneo la Mabatini ambako
ulitarajiwa kuzikwa leo mchana (Jumamosi).
No comments:
Post a Comment