Shule za umma za sekondari zimeamrishwa kufungwa katika jimbo la Yobe
Kaskazini mwa Nigeria baada ya mauaji ya halaiki ambayo wapiganaji wa
kiisilamu wanashukiwa kuwaua wanafunzi 22 na kuiteketeza shule yao.
Gavana wa Yobe, Ibrahim Gaidam amelaani mashambulizi hayo yaliyofanyika Jumamosi katika shule la Mamudo na kuyaita ya kinyama.
Nigeria imelaumu wapiganaji wa kiisilamu wa Boko Haram, waliolenga kushambulia shule mbili katika eneo hilo mwezi Juni .
Tafsiri ya jina Boko Haram, inamaanisha elimu ya kimagharibi imeharamishwa.
Mamia ya shule zimeteketezwa na wapiganaji wa kiisilamu tangu mwaka 2010.
Alipoitembelea shule hiyo Jumapili, bwana Gaidam aliwataja washambulizi kama watu wasioheshimu utu.
Aliamuru shule za umma kufungwa hadi mwanzo wa
muhula mpya wa shule mwezi Septemba, ili kuruhusu serikali ya majimbo
pamoja na maafisa wa serikali kuangalia njia za kuhakikisha usalama
katika shule za umma.
Pia aliitaka serikali kuondoa marufuku iliyowekewa upeperushaji wa masafa ya simu za mkononi katika jimbo hilo.
Yobe ni moja ya majimbo ambako rais Goodluck
Jonathan alitangaza sheria ya hali ya hatari mwezi Mei na kuwapeleka
mamia ya majeshi katika eneo hilo.
Walioshuhudia tukio hilo walisema baadhi ya
wathiriwa wa shambulizi waliteketezwa wakiwa hai katika shambulizi la
Jumamosi wakati wengine wakipigwa risasi walipokuwa wanakimbilia usalama
wao.
Wazazi walikuwa na wakati mgumu kutambua miili ya wanao iliyoteketezwa kiasi cha kutotambulika.
Walionusurika walisema kuwa watu wanaoshukiwa
kuwa wapiganaji wa kiisilamu waliwasili katika shule hiyo wakiwa na
mafuta ya petroli kwa wingi tayari kuiteketeza shule.
Wale waliojeruhiwa kwenye shambulizi hilo walipokea matibabu ya bure.
HABARI HII NI KWA HISANI YA SHIRIKA LA HABARI LA UINGEREZA IDHAA YA KISWAHILI BBC
No comments:
Post a Comment