Thursday, March 29, 2018

WARAMI:CHADEMA WASIINGILIE UHURU WA MAHAKAMA

Na Mwandishi Wetu
WATETEZI wa Rasilimali Wasio na Mipaka(Warami)limesema limesikitishwa na kitendo cha Kamati kuu ya   Chadema kuingilia uhuru wa Mahakama baada ya jana kuitisha mkutano kuzungumzia mambo yalipo mahakamani.

Warami wameongeza kuwa  si tu kuingilia uhuru wa mahakama pia chama hicho kimekwenda mbali zaidi kwa kutoa masharti yanayoashiria uvunjifu wa amani iwapo Mwenyekiti wa Freeman Mbowe na viongozi wengine watanyimwa dhamana leo.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam Mkurugunzi wa Utafiti wa Warami Philipo Mwakibinga amesema jana baadhi ya viongozi wa Chadema kupitia mkutano wao wameonesha dhahiri kuingilia uhuru wa Mahakama kwa kuanza kushinikisha maamuzi ya Mahakama.

“Mbunge wa Arusha Mjini Godbles Lema, Profesa Abdallah Safari na wenzao wakiwa wanajua kuwa Mahakama ni chombo cha haki walitengeneza mazingira ya kuonesha kuwa viongozi hawatetendewi haki kama hawatapa dhamana leo.

“Wanafanya hivyo wakijua wazi jambo hili limelenga kuishawishi , kushinikiza na kuilazimisha mahakama ifanye watakavyo wao kwa kuacha misingi ya haki wajibu na maadili ya kimahakama,”amesema Mwakibinga.

Amefafanua Watanzania ni mashahidi Mbowe na wenzake ambao wapo Mahakamani wamekamatwa kama matokeo ya matendo yao ya kushawishi na kuchochea chuki miongoni watanzania jambo ambalo si la kiutamaduni kwa Taifa.
“Warami tunapenda kuwakumbusha Watanzania kuwa sheria ni kama kaa la moto  na unapovunja sharia lazima ujue umeamua kushika kaa la moto kwa hivyo lazima ujiandae kuungua.

“Tunawakumbusha Chadema ,hasa wakina Lema na wenzao watii sheria , waache maneno ya kichochezi yasiyo ya kiuongozi na wasiendelee kuropoka ropoka, zama za kuwachekea waropokaji zimepitwa na wakati,”amesema.

Mwakibinga amesema Lema kukamatwa kwa viongozi wa chama chake ni mkakati uliopangwa na Serikali kwa ajili ya kuwakomoa.

Amesema Warami wanawapa changamoto Chadema , wamuulize Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye ajitokeze hadharani wakati Augustino Mrema akiwa NCCR-Mageuzi na baadae TLP alivyokuwa anakamatwa na vyombo vya dola je alikuwa analazimisha vyombo vya dola vimkamate wakati Mrema hakuwa na makosa kwa wakati ule.

“Chadema waache kuharibu sifa ya vyombo vyetu vya kiusalama  hasa idara nyeti ya Usalama wa Taifa kwa kuwasingizia mambo ya ajabu ajabu kwa ajili ya kuficha udhaifu wao wa kuimarisha chama,”amesema Mwakibinga.

Ameongeza Warami inawataka Chadema kuacha kukimbia kivuli chao na waswahili wanasema ‘ukilikoroga lazima ulinywe’ .

“Hivyo Chadema walinywe kwa kadiri ya walivyorikoroga.Pia iache Mahakama itafisiri sheria na kwa kuwa wameweka wanasheria wanaowaamini, wawahimize wanasheria wao kuhakikisha wanashinda kesi zinazowakabili,”amesisitiza.

KUHUSU MAASKOFU KUTUMIKA

Mwakibinga amesema mara ya mwisho walihoji iwapo maaskofu wanatumika na vyama vya siasa hasa Chadema.

“Nafikiri wote sasa tumejiridhisha kuwa maaskofu wetu wameamua kutumika kulipa fadhila za waliokuwa wanawapa fedha katika zama za kufanya harambee ya fedha kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2015.

“Matukio ya Chadema kuunga mkono hadharani waraka wa maaskofu ,ACT Wazalendo kunifukuza uanachama kwa mimi kuwakosoa maaskofu na Maalim Seif kutangaza hadharani anaunga mkono madudu yale ya maaskofu,”amesema.

Ameongeza hivyo ni vishiaria na kuthibitisha wazi maaskofu wameamua kutumika na kuyaacha maelekezo na mafunzo ya dini yanayotaka kilicho cha kaisari apewe kaisari na kilicho cha Mungu apewe Mungu.
Ametumia nafasi hiyo kuwaasa wanasiasa, wanaharakati , wanahabari , viongozi wa dini , taasisi binafsi  waanzishe utaratibu wa kuheshimu uhuru wa Mahakama na kutoa kauli za mashinikizo.
 Mkurugenzi wa Utafiti kutoka Watetezi wa Rasilimali wasio na Mipaka (WARAMI),Philipo Mwakibinga , akizungumza na Waandishi wa habari  kuhusu mkutano wa  Kamati Kuu ya Chadema uliofanyika jana ukiwa na lengo la kuingia uhuru wa Mahakama.
 Mkurugenzi wa Utafiti kutoka Watetezi wa Rasilimali wasio na Mipaka (WARAMI),Philipo Mwakibinga, akiwaeleza jambo waandishi wa habari yaliyojiri katika mkutano mkuu wa Chadema.


No comments:

Post a Comment