Tuesday, March 20, 2018

JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI LATOA TAADHARI KWA MATUKIO YA MOTO

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Kufuatia uwepo na muendelezo wa matukio ya moto katika maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwemo shule za bweni, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linatoa tahadhari kwa Wanafunzi, Wakuu wa Shule, Wamiliki na Wananchi kwa ujumla kuchukua tahadhari kwa kuwa makini katika matumizi ya vifaa vya umeme.

Msemaji wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkaguzi (INSP) Joseph Mwasabeja (Pichani kushoto) amesema, kutokana na matukio haya ya moto kutokea mara kwa mara katika Jamii yetu hususani katika Shule za Bweni hasa Shule za Sekondari na kusababisha uharibifu wa miundombinu kama vile mali, majengo na wakati mwingine majeraha au vifo kwa wanafunzi wetu. Mara nyingi matokeo ya majanga haya huleta hasara na sintofahamu kwa Wananchi na Taifa kwa ujumla.

Amesema, uchunguzi wa moto ( Fire Investigation) umebaini sababu za matukio hayo ni matumizi mabaya ya umeme yanayofanywa na wanafunzi kwa kujiunganishia nyaya za umeme wenyewe bila ya kuwa na weledi ili wapate sehemu za kuchaji simu na heater za kuchemshia maji kwa kificho kwasababu wanafunzi hawaruhusiwi kuwa na simu wala heater pindi wanapokuwa Shuleni.


Aidha, majanga ya moto yamekuwa yakitokea katika jamii yetu, kwasababu moto ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Pia ni wazi kuwa na vyanzo vingi vya moto ni sisi wenyewe (binadamu) kutokana na uzembe au hujuma.

Ili kupunguza matukio haya Jeshi letu limeanzisha ( Fire Klabu) kwa Shule za Msingi na Sekondari, hatua itakayosaidia kuwapa Elimu Stahiki ya kukabiliana na majanga ya moto na hatimaye kuwa na mabalozi wa Zimamoto na Uokoaji katika Shule na makazi yao.

Wito wangu kwa wamiliki wa Shule walipokee jambo hili kama ukombozi kwao ili kupunguza majanga na madhara ya moto pindi unapotokea katika Shule zao. Pia amewataka Wamiliki wa Shule kuzingatia maelekezo na ushauri unatolewa na Jeshi letu juu ya Kinga na Tahadhari dhidi ya majanga ya Moto.

“Vilevile niwaombe wananchi wote kuwa wepesi katika kutoa taarifa pindi wanapopata majanga ya moto na majanga mengine kwa kupiga namba 114 ili Askari wetu waweze kufika kwa wakati na kuokoa Maisha na Mali. Alisema huku akiwashauri wananchi kuwa na Vifaa vya kuzimia moto (Fire Extinguisher). ’’
Imetolewa na;





Joseph Mwasabeja – Mkaguzi Msaidizi (INSP)
Msemaji wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji
Makao Makuu
20 Marchi, 2018



No comments:

Post a Comment