Tuesday, February 13, 2018

SERIKALI KUONDOA VIKWAZO KATIKA UWEKEZAJI

Jonas Kamaleki- MAELEZO

Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa kushirikiana na wadau wanaohusika na uwezeshaji wa uwekezaji nchini wamejipanga kuondoa ama kupunguza ukiritimba katika utoaji vibali kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Hayo yamebainishwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Geofrey Mwambe (PICHANI KULIA) katika mahojiano maalum na Idara ya Habari (MAELEZO) jijini Dar es Salaam.

Mwambe amesema kuwa mashirika na taasisi mbali zinazohusika na utoaji vibali kwa wawekezaji ikiwemo, Idara ya Kazi, Uhamiaji, Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Baraza la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na wadau wengine wameazimia kuangalia sheria zao na kuainisha maeneo yanayokwamisha uwekezaji na kuyafanyia kazi mara moja.

“Tutumie Sheria katika kufikia malengo na sio kukwamisha uwekezaji, ili tuweze kufikia uchumi wa kati unaotokana na viwanda,”alisema Mwambe. Aidha, Mwambe amesema vibali vya uwekezaji vitolewe kwa muda mfupi ili kuvutia wawekezaji wa ndani nan je ya nchi.
Amesema hati ya umiliki wa ardhi kwa ajili ya uwekezaji itolewe kwa wakati ili kumwondelea mwekezaji usumbufu unaoweza kujitokeza, kwa kufanya hivyo wawekezaji wataongezeka na hivyo kujenga viwanda vingi ambavyo vitaongeza ajira hasa kwa vijana.

Katika kuhakikisha uwekezaji nchini unarahisishwa, kimeanzishwa kituo kimoja cha kutolea huduma zinazohusu uwekezaji (One stop Centre) katika ofisi za TIC. Hii inamrahisishia mwekezaji kupata huduma zote sehemu na hivyo kumuondolea bughdha ya kupoteza muda.

Kwa mujibu wa Mwambe, TIC inatafuta pia namna bora ya kulipia vibali mbali mbali vya uwekezaji katika sehemu moja na malipo hayo kupelekwa katika ofisi husika kwa njia ya kielektroniki.

Zipo hatua nyingine nyingi zinazochukuliwa ili kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya uwekezaji. Mpaka sasa TIC kwa kushirikiana na taasisi na mashirika mbali mbali ya Serikali wameshaondoa vikwazo 53 vya uwekezaji.

Ikumbukwe kuwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amekuwa akisema kuwa hataki ukiritimba na zile kauli za “njoo kesho”, “tuko kwenye mchakato” au “tutalishughulikia”. Kwa kuzingatia hilo TIC kwa kiwango kikubwa imeondoa na inaendelea kuondoa ukwamishaji katika eneo la uwekezaji.

Kamati ya Taifa ya Huduma kwa Wawekezaji inaendelea kutafuta njia ya kuhakikisha inapunguza vikwazo ama urasimu katika uwekezaji nchini ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kujenga uchumi wa viwanda.

No comments:

Post a Comment