Tuesday, February 13, 2018

ELIMU KWA WAFUGA NYUKI KUMEONGEZA UZALISHAJI ASALI

NA TIGANYA VINCENT
RS-TABORA

SERIKALI ya Mkoa wa Tabora imesema mafunzo ambayo yanayotolewa kwa wafugaji wa nyuki hapa nchini yamesaidia kuongezeka uzalishaji wa mazao ya asali na hivyo kuwepo na uwekezaji katika biashara ya mazao ya nyuki.

Hatua hiyo imetokana kuwepo kwa soko kubwa dunia la mazao ya nyuki ambalo limefanya kuwepo na chachu kufungua mianya ya wafugaji na wafanyabiashara kutaka kujifunza juu ya uzalishaji unaoazingatia ubora na unaokubalika kitaifa na kimataifa.

Kauli hiyo jana na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Nathilis Linuma wakati akifungua mafunzo ya siku tano ya wafanyabiashara wa biadha zinazotokana na nyuki katika Chuo cha Nyuki na kuwashirikisha washiriki kutoka Mwanza, Simiyu na wenyeji.

Linuma alisema takwimu zinaonesha kuwa uzalishaji wa mazao ya nyuki hususani asali na nta unaongezeka kutoka tani 9,000 za asali kwa mavuno ya mwaka 2012 hadi tani 34,000 za asali kwa mavuno ya mwaka 2016 .

Aliongeza kwa mauzo ya nje ya asali yalikuwa tani 103.8 mwaka 2012 na kufikia tani 259.9 kwa mwaka 2016 yenye thamani ya Shilingi 2,257,410,880.

Linuma alisema kwa upande wa nta mwaka 2012 iliuzwa tani 277 ambapo hakukuwa na ongezeko na kasi kilichouzwa mwaka 2016 ilikuwa ni tani 251.9 yenye thamani ya Shilingi 4,549,643,832.

Kaimu Katibu Tawaka huyo wa Mkoa alisema kuwa ongezeko hilo la uzalishaji linatokana na mwitikio wa wananchi kupata elimu ya ufugaji wa kisasa na kuwekeza katika mashamba ya ufugaji nyuki nchini.

Aidha alisema kuwa ili uzalishaji uendelee kuongezeka ni vema wafugaji na jamii wakaendelea kuhakikisha wanatunza mazingira na kupanda miti kwa wingi ili nyuki wapate chakula cha kuzalishia asali na pia wasaidia mimea mashambani.

Kwa upande wa Mkuu wa Chuo cha Ufugaji Nyuki Tabora Semu Daud alisema wameamua kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa wafugaji mbalimbali hapa nchini kwa lengo la kuhakikisha kuwa bidhaa wanazozalisha zinakubalika ndani na nje ya Tanzania.

Alisema wanashirikiana na Shirika la Viwango Tanzania(TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa(TFDA) ili kuhakikisha mazao yanayozalishwa yanakuwa yanaviwango viwango vinakubalika na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kwa ajili ya kuwatafutia masoko ndani na nje ya Tanzania.

Tanzania ina maeneo makubwa ambayo ufugaji nyuki unatekelezwa, baadhi ya mikoa hiyo ni pamoja na Dodoma, Singida, Shinyanga, Tabora, Kigoma, Simiyu, Mwanza, Katavi na Kagera ambayo inapitiwa na barabara iendayo Burundi, Rwanda na Uganda, barabara hii ni fursa kwa mazao ya nyuki kuelekea soko la nchi jirani.

No comments:

Post a Comment